Monday, 20 March 2017

SERIKALI YAWATOA HOFU WAZANZIBAR


RAIS Dk. John Magufuli, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, ilisema kuwa mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Kahitwa Bishaija na Meneja Mwandamizi wa Fedha wa TANESCO, Sadock Mugendi.

Wakati huo huo, taarifa ilisema Profesa Muhongo aliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa, hawatakatiwa umeme baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kuanza kulipa deni inalodaiwa na TANESCO.

Profesa Muhongo alisema tayari SMZ, imeanza kulipa kiasi cha sh. bilioni 10, na itaendelea kulipa deni hilo mpaka litakapomalizika.

Aidha, Profesa Muhongo alitoa wito kwa wadaiwa sugu wote wa TANESCO, kulipa madeni yao katika kipindi cha siku tano zilizobaki kwa kuwa wasipolipa watakatiwa umeme.

Hivi karibuni, Rais Dk. Magufuli aliitaka TANESCO kudai wateja wake kulipia bili za umeme na kwamba, ikibidi wawakatie huduma hiyo.

Kutokana na agizo hilo, TANESCO ilitangaza kutoa wiki mbili kwa wadaiwa wote sugu, kulipa madeni yao na kwamba, baada ya kipindi hicho kumalizika, wadaiwa wote watakatiwa umeme.

SMZ ni miongoni mwa wateja waliotangaziwa kudaiwa fedha nyingi na TANESCO.

No comments:

Post a Comment