Wednesday 22 March 2017

UTATA WAZUKA KORTINI MAHALI ALIKO MANJI


SUALA la mfanyabiashara maarufu Yussuf Manji, kudaiwa kushikiliwa akiwa Hospitali ya Aga Khan, limeibua sintofahamu baada ya upande wa Jamhuri kuieleza Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kwamba hashikiliwi.

Wakati Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Oswald Tibabyekomya, akiieleza mahakama hiyo jana, kwamba mfanyabiashara huyo hashikiliwi,  mawakili wake walidai mteja wao huyo alifikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa Idara ya Uhamiaji na askari polisi.

Kutokana na hilo, Jaji Ama-Isario Munisi, ameamuru mfanyabiashara huyo, ambaye alikuwa nje kwa dhamana aliyopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai namba 63 ya mwaka huu, aendelee kukaa nje huru chini ya masharti aliyokuwa amepewa na mahakama hiyo.

Hayo yalijitokeza mahakamani hapo, wakati maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na Manji kupitia mawakili wake, Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Jeremiah Ntobesya, yalipopelekwa kwa kusikilizwa.

Manji kupitia mawakili wake hao, aliwasilisha maombi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam na Idara ya Uhamiaji, ambapo alikuwa akipinga kushikiliwa isivyo halali na kuomba tuhuma zinazomkabili zishughulikiwe kwa mujibu wa sheria.

Mawakili wa mfanyabiashara huyo, walieleza kuwa mleta maombi (Manji), amefika mahakamani hapo.

Baada ya kueleza hayo, Tibabyekomya alidai wamewasilisha hati za viapo tatu na wamewashawapatia mawakili wa Manji, ambapo vimeeleza kuwa hashikiliwi.

Wakili Mgongolwa alidai Manji amefika mahakamani hapo akitokea hospitali ya Aga Khan, akiwa ameambatana na maofisa uhamiaji na polisi ambao walikuja na gari lingine.

Alidai askari hao walipojua kwamba shauri hilo limepelekwa kwa usikilizwaji, waliamua kuishia nje na wamekuwa wakilala hospitalini.

Wakili huyo alidai miongoni mwa viapo vilivyopo hapo, kipo cha Ofisa Uhamiaji, Anord Munuo, ambaye ameeleza aliandika maelezo ya Manji, Februari 20, mwaka huu, lakini hakupewa dhamana.

Hata hivyo, Tibabyekomya alidai anachoeleza Mgongolwa hakipo katika hati ya kiapo, kwani Manji hayuko kizuizini kwa kuwa tangu Februari 27, mwaka huu, alipoachiliwa kwa dhamana Kisutu, hayupo katika mikono ya polisi.

Wakili Ndusyepo alidai Manji anashikiliwa kwa takriban siku 30, akiwa katika Hospitali ya Aga Khan.

Jaji Munisi alionyesha kushangazwa na maelezo yanayotolewa mahakamani hapo na mawakili hao na kutaka kujua ukweli juu ya jambo hilo.

“Upande wa Jamhuri unadai hashikiliwi, hawa wanadai anashikiliwa, nataka kujua nani kati yenu anasema ukweli,” alisema Jaji Munisi.

Wakili Mgongolwa aliendelea kusisitiza kwamba, Manji anashikiliwa na amepelekwa mahakamani hapo chini ya ulinzi, kauli ambayo iliungwa mkono na msaidizi wa Manji, aliyekuwepo mahakamani hapo, ambaye alieleza kuwa maofisa hao wametoka nao hospitalini, lakini walipofika hapo waligoma kupanda juu.

Baada ya hapo, mawakili wa Manji waliomba wapatiwe muda ili waweze kuwasilisha majibu ya hati iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri na mahakama iingize katika kumbukumbu zake kwamba, mfanyabiashara huyo hajashikiliwa.

Tibabyekomya alidai katika hati za viapo zote tatu walizowasilishwa mahakamani hapo, zinaeleza Manji hashikiliwi na Idara ya Uhamiaji.

Mgongolwa alidai Ofisa Uhamiaji Munuo alimuita Manji kwa ajili ya kumhoji juu ya tuhuma za kuishi nchini isivyo halali na kutoa taarifa za uongo na kuelezwa mashitaka yanahitaji kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

“Ndusyepo alipokuwa akifuatilia Idara ya Uhamiaji, walikuwa wakimjibu hivyo. Katika majibu yetu, tutaleta ushahidi kutoka kwa maofisa wa hospitali ya Aga Khan, kuelezea hilo na madereva.

“Sisi sio wendawazimu wa kuleta maombi haya mahakamani. Tutaleta vielelezo na tutathibitisha hilo, tusingekuwa na sababu  ya kuleta kwamba, mtu anashikiliwa wakati hashikiliwi,” alidai Mgongolwa.

Jaji Munisi aliwakata mawakili wa Manji, kupeleka mahakamani hapo kile kinachotakiwa ili awasilikize. Aliwaamuru mawakili hao kuwasilisha majibu ya hati ya viapo kinzamni Machi 24, mwaka huu na maombi hayo atayasikiliza Machi 27, mwaka huu.

Baada ya kuahirishwa kwa maombi hayo, Manji aliondoka mahakamani hapo kwa kutumia teksi, akiwa na msaidizi wake na kuingia katika Hoteli ya Hyatt.

No comments:

Post a Comment