Wednesday 22 March 2017

MWIGULU AWAVAA POLISI SAKATA LA BODABODA


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amezindua Bodi ya Parole na kuvitaka vyombo vya ulinzi kuacha kugeuzi madereva bodaboda kuwa mradi huku akisisitiza kuacha urasimu katika vituo vya polisi.

Aidha, ametaka madereva hao na watu wengine wanapokamatwa upelelezi ufanywe kwa wakati na wanapoonekana kuwa hawana hatia waachiwe haraka ikibidi hata kuombwa radhi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuzindua Bodi ya Parole,Waziri Mwigulu, alisema hatua hiyo ikizingatiwa itapunguza msongamano katika magereza na kuwapa haki wanaochukuliwa hatua bila hatia.

Alisema ni vizuri kwa watu ambao polisi wamejiridhisha hawana hatia kuachiwa huru ikibidi kuombwa msamaha.

“Isiwe tabu mtu kutoka kituoni, natoa maelekezo mwenye makosa ni vizuri kufika kwenye  vyombo vya sheria, lakini mkijiridhisha hana hatia mwachieni isiwe polisi kuingia rahisi kutoka tabu hasa kwa bodaboda, tusidhani uwepo wao ni mradi sitaki hiyo dhana,”alisema.

Mwigulu alisema ustaarabu wa nchi zote duniani hupimwa kwa kuzingatia namna serikali inavyoshughulikia uhifadhi na urekebishaji wa wahalifu gerezani, hivyo bodi hiyo ishirikishe jamii katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema pamoja na changamoto zilizojitokeza katika uanzishwaji na utekelezaji wa Mpango wa Parole kwa kuwapo na idadi ndogo ya wafungwa walionufaika kumekuwapo na raia wema na ushiriki wa ujenzi wa taifa kwa wanufaika hao.

“Kati ya wafungwa 4,815 walionufaika na mpango wa Parole ni wafungwa 25 tu walikiuka masharti, hivyo huu ni ushahidi kuwa mpango huu ukisimamiwa na kutekelezwa ipaswavyo utasaidia kurekebisha na kupunguza uhalifu,”alisema.

Alisema Bodi hiyo ina ufinyu wa bajeti,vitendea kazi na ufinyu wa wigo wa sheria katika kuwezesha wafungwa wengi katika mpango kazi na serikali inafanyia kazi na kutafuta ufumbuzi wa kudumu.

Akizungumzia hatua ya uhalifu katika baadhi ya maeneo ikiwemo mkoani Pwani, alisema tayari amemuagiza Naibu Waziri Hamad Masauni kufika eneo la tukio jana na kuchukua hatua.

Alisema tayari baadhi ya wanaodhaniwa kuhusika katika uhalifu huo wametiwa mbaroni na hatua zaidi zinachukuliwa ikiwemo kufanyia kazi ushauri wa wakazi hao katika kumaliza tatizo la wafugaji na wakulima.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Augustino Mrema alisema kundi kubwa la wahalifu waliopo gerezani ni vijana wa bodaboda,watumiaji dawa za kulevya,dada poa na kaka poa ambao wakipatiwa elimu stahiki wengi watabadilika na kuacha uovu huo.

Alimwomba Mwigulu kufanyia kazi hatua za michakato ikiwemo ya wafungwa wanaohitajika kupatiwa msamaha na Parole, lakini bado kuna vikao na taarifa za wafungwa zinasubiriwa kutoka katika jamii na familia walikozaliwa.

Alisema Bodi hiyo inaunga mkono hatua ya wafungwa kushirikishwa katika kazi za umma na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na wajumbe walioteuliwa.

Kwa upande wake,Katibu wa Bodi hiyo,Dk. Juma Malewa alisema tangu bodi hiyo kuanza kazi wafungwa 5495 wamejadiliwa, wafungwa 4815 wamenufaika na wafungwa 680 wamekataliwa kwa sababu mbalimbali.

Alisema vikao 33 vimefanyika na kutokana na mtazamo wa kimataifa kuhusu sera endelevu ya urekebishaji wa wahalifu unasisitiza ushirikishaji wa jamii.

No comments:

Post a Comment