Saturday, 5 March 2016

WATAKAOHARIBU, HAWATAHAMISHWA-MAJALIWA




NA MWANDISHI MAALUMU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema watumishi wa umma wako huru kuhamia kokote wapendako, lakini wahakikishe wanakwenda huko wakiwa safi na kamwe mtu asiharibu kazi akitarajia kuwa atahamishiwa sehemu nyingine.

“Serikali hii haina utumishi kwa mtu aliyeharibu kazi. Usije ukaharibu hapa Itilima ukadhani utaenda Bunda kuendelea na kazi. Serikali ya awamu hii haina nafasi na watumishi wa aina hiyo,”amesema.

Waziri Mkuu alitoa onyo hilo  jana, wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Itilima, kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambao aliuzindua.

“Watumishi wenzangu huu ni wakati wa kubadilika na kuona mwelekeo wa serikali hii ya awamu ya tano ukoje. Jukumu letu ni kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao, rangi wala dini zao,”alisisitiza.

Waziri Mkuu aliwahakikishia watumishi hao kwamba serikali inatambua changamoto walizonazo kutokana na upya wa wilaya hiyo na mkoa huo na akawaahidi kuwa itaboresha mazingira yao.

“Msiwaadhibu wananchi kwa kisingizio cha mazingira magumu ya kazi zenu, tunajua mnayo madai ya nauli, posho za mafunzo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya likizo,” alisema huku akishangiliwa.

Alisema serikali itayalipa madeni hayo japo haitamaliza yote kwa wakati mmoja, lakini aha hakika wa kukamilishwa walau kwa asilimia 80.

Mapema akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Georgina Bundala, alisema ilianzishwa Machi, 2012 na kupata halmashauri Julai, 2013.

Alisema kwa sasa wilaya hiyo haina kituo cha polisi cha wilaya, haina gereza, ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mahakama ya wilaya na benki.

Mkuu huyo wa wilaya alisema pia haina hospitali ya wilaya, lakini
alibainisha kuwa wamekwishatenga eneo la ekari 30 kwa ajili ya ujenzi huo.

“Pia tumekwishapima viwanja 123 na eneo la kujenga  taasisi lenye ekari 143.8, limefanyiwa uthamini na fidia kukamilika,” alisema.

No comments:

Post a Comment