Saturday, 5 March 2016

WIZI MKUBWA WABAINIKA SOKO LA ILALA


SERIKALI imebaini upotevu wa mapato kwenye soko la vyakula la Ilala, Boma, Dar es Salaam, ambako zaidi ya asilimia 60 ya ushuru unaokusanywa unadaiwa kuingia kwenye mifuko ya watu binafsi.

Ubadhirifu huo unafanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika vya wafanyabiashara hao, kwa kutoza viwango tofauti vya ushuru visivyofuata utaratibu kwa kutumia risiti tofauti, ambazo sio za kieletroniki.

Kufuatia hali hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Isaya Mngurumi, ameagizwa kukutana na wafanyabiashara hao katika kipindi cha wiki tatu na kuandaa utaratibu rasmi utakaotumika kwenye ukusanyaji wa mapato hayo.

Aidha, imetoa onyo la kuwachukulia hatua kali za kisheria, yeyote atakayethubutu kuwatisha au kuwafukuza wafanyabiashara waliobainisha kero na ubadhirifu uliopo sokoni hapo.

Hayo yalibainika jana, wakati Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora, Suleiman Jaffo, alipofanya ziara kwenye soko hilo, ambapo alishuhudia ubovu wa miundombinu ya majitaka huku uongozi wa soko hilo ukionekana dhahiri kushindwa kutatua kero za wafanyabiashara.

Jaffo alisema ushuru unaokusanywa na vyama vya ushirika  hauendani na vipato halisi vya wafanyabiashara na kubainisha kuwa, mapato hayo yamekuwa yakiingia kwenye mifuko ya watu binafsi.

Alisema licha ya manispaa kukusanya kodi ya sh. 300 kwa siku kwa kila wafanyabiashara, lakini vyama hivyo vimekuwa vikikusanya hadi sh. 30,000.

“Ushuru unaokusanywa na vyama vya ushirika, asilimia 60 ya mapato yake hayaingii serikalini, kutokana na kukusanywa bila utaratibu maalumu. Huu unaonekana ni mkakati wa watu wachache kujinufaisha,”alisisitiza.

Pia,  alibaini kuwepo kwa baadhi ya mabanda ya mama lishe kuhodhiwa na watu, ambao wamekuwa wakiwatoza kodi ya sh. 80,000 kwa mwezi, licha ya wao kuilipa manispaa ushuru wa sh. 9,000 kwa mwezi.

Hivyo, aliagiza kufanyika kwa uhakiki wa wafanyabiashara hao ili kubaini watu waliohodhi vibanda hivyo.

Kufuatia maagizo hayo, Mkurugenzi wa manispaa hiyo, alisema tayari wameanza kufanya uhakiki pamoja na kuanza mipango ya kuboresha soko hilo.

Kwa upande wa wafanyabiashara hao, walilalamikia kubadilishwa kwa makandarasi wanaokusanya mapato hayo mara kwa mara.

Kitwana Mohamed, alisema mabadiliko ya mara kwa mara kwa makandarasi wa kukusanya ushuru, yanatia shaka kutokana na  kutoshirikishwa kwa wadau wa soko hilo pindi uamuzi unapofanyika.

Alisema serikali inapaswa kuufanyia mabadiliko uongozi wa soko hilo ili kuhakikisha mapato yanayokusanywa yanatumika kuboresha miundombinu ya sokoni hapo.

No comments:

Post a Comment