Saturday, 5 March 2016
MAJIPU SITA YATUMBULIWA, MATANO WIZARA YA MALIASILI NA UTALII, MMOJA MUUGUZI
SERIKALI imeendelea kukunjua makucha baada ya kuwasimamisha kazi watumishi watano wa idara ya uhasibu katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na kuwahamishia wizarani wafanyakazi 15.
Watumishi hao wamesimamishwa kazi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, kwa kosa la kufungua akaunti katika Benki ya Exim, jambo ambalo amesema ni kinyume cha utaratibu na sheria zinazoongoza utunzaji na uhifadhi wa fedha za serikali.
Profesa Maghembe alichukua uamuzi huo jana, baada ya kulazimika kufanya ziara ya siku moja ya kushtukiza, katika ofisi za mamlaka hiyo, zilizoko wilaya ya Ngorongoro mkoani hapa, baada ya kupata taarifa juu ya ukiukwaji wa sheria uliofanywa na baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo.
Watumishi waliosimamishwa kazi kutoka Idara ya Uhasibu ni Maria Njau, Joseph Ntwala, Ally Amiri, Joseph Msafiri na John Mlambo.
Waliohamishwa vituo vya kazi na kupelekwa wizarani ni Meneja Mipango, Joseph Mshana, Kaimu Meneja wa Ikolojia Patrice Matay na Injinia Isra Misana, ambaye ni Meneja wa Eng. Services.
Wengine ni Amina Ponera, Richard Hyri kutoka Idara ya Utalii, Agatha Ambroce na Lukoba Lyambogo, ambao ni wahasibu, Charles Mayuya, ambaye ni PMU, Edmund Sabutoke, ambaye ni Mtunza Stoo ,Fanuel Mfinanga na Jonathan Mugisha, wanaotoka Idara ya Mipango na Fedha.
Pia wamo Esther Makacha, ambaye ni Katibu Muhtasi,Rebecca Missoji, ambaye ni Msajili, Emanuel Nyangaro, ambaye ni Ofisa Uhifadhi na Francis Kone, ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mamlaka hiyo.
Profesa Maghembe amemwagiza Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Fredy Manongi, kuandika taarifa ya watumishi hao, ambao wanatambua wazi sheria haiwaruhusu kufanya hivyo, lakini walithubutu bila ya kuhofia ajira zao.
“Nataka ikifika Jumatatu ya wiki kesho (Jumatatu ijayo), nipate maelezo ya kina ya maandishi kwa nini mliamua kufungua akaunti zenu binafsi katika Benki ya Exim wakati siyo benki rasmi ya kuweka fedha za mamlaka.
“Kuna watumishi wa mamlaka hapa nasikia mna tabia ya kupika majungu, uvivu, ujanja ujanja na fitina katika utendaji wa shughuli za ofisi, naomba tabia hiyo ikome, fanyeni kazi kwa bidii kwani majungu hayatawasaidia chochote katika utendaji wenu,”alisema.
Kwa upande wake, Manongi alimwambia Profesa Maghembe kuwa, kuna tabia ya baadhi ya watumishi kutoka vyombo vya dola, kukwamisha shughuli za ofisi kwa kuwaita watumishi wa mamlaka na kwenda kuwahoji kutokana na tuhuma mbalimbali ambazo hazina ushahidi.
Wakati huohuo, Peter Katulanda ameripoti kutoka Mwanza kuwa, sakata la watoto waliofariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, iliyoko Butimba jijini Mwanza, limechukua sura mpya baada ya Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Nangi William, kushushwa madaraka wakati Muuguzi Mkuu, Suzan Lumash, amesimamishwa kazi.
Kusimamishwa kazi kwa Suzan kunatokana na kushindwa kuwasimamia wataalamu na watumishi wakati wa utoaji huduma kwa wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo.
Akizungumza kwenye kikao cha pamoja baina ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, alisema uzembe wa aina hiyo hauvumiliki.
Mulongo alisema kufuatia tukio hilo, lililotokea Jumatano iliyopita katika hospitali hiyo, aliunda tume ya watu watano, ambayo mwenyekiti wake alikuwa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Rweyendela Onesmo, ilipendekeza kumshusha madaraka Dk. Wiliam.
“Kuanzia sasa Dk. William umeshushwa madaraka yako uliyokuwa nayo kama Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Butimba, utakuwa daktari wa kawaida na Muuguzi Mkuu, Lumash (Suzan) wewe utasimama kazi kupisha uchunguzi wa tume niliyoiunda,” alisema.
Aliiagiza tume hiyo kuchunguza kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wagonjwa wanaofika kupata huduma za afya hospitalini hapo, madai ya wataalamu, wauguzi na watumishi kutumia maneno yasiyofariji wagonjwa, uzembe na huduma zinazotolewa kudaiwa kuwa duni.
Kwa mujibu wa Mulongo, tume hiyo itawasilisha taarifa yake Jumatatu ijayo, ili hatua nyingine zaidi zichukuliwe na kuwaomba wananchi wa wilaya hiyo na jiji la Mwanza, waendelee kupata huduma katika hospitali hiyo bila hofu kwani serikali ya awamu ya tano ni ya kazi na sio lelemama.
Kutokana na hatua hiyo, madaktari na wauguzi waliotumbuliwa majipu hospitalini hapo wamefikia wanane. Wengine ni Ngusa Masanja, Dk.Noorne Jandwa, Dk. Emeriana Mvungo na wauguzi ni Suzan Sindano, Maria Mkankule, Bibiana Moshi na Janeth Foya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment