Friday, 4 March 2016
CCM SIMIYU WAMPA TANO MAJALIWA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Simiyu,
kimempongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutokana na ujasiri alionao wa kutumbua majipu, jambo lililosababisha wananchi kurudisha imani kwa serikali yao.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa, Dk. Titus Kamani, katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi, kwenye viwanja vya Lamadi wilayani Busega, ambao ulihudhuriwa na Waziri Mkuu, Majaliwa.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa wa watu, Dk. Kamani alisema mafuriko hayo ya wananchi kwenye mkutano huo yametokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
Alisema ujasiri aliokuwa nao Majaliwa wa kushughulikia wakwepa kodi, wala rushwa na wabadhilifu wa mali za umma, umesababisha wananchi wengi kuwa na imani kubwa kwa serikali na hata uchaguzi ukifanyika Chama kitashinda kwa kishindo.
Dk. Kamani alisema mikakati ya serikali ya kusimamia mapato na kuwabana wakwepa kodi, itawezesha taifa kujiendesha lenyewe bila ya kutegemea misaada ya wafadhili.
Alisema Chama mkoa kitaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha inafikia malengo ya kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo kwa kuhakikisha Ilani inatekelezwa kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Raphael Chegeni, alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidi kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya karibu na maeneo yao.
Waziri Mkuu aliwashukuru wakazi wa Busega kwa imani waliyokuwa nayo kwa serikali na kuwaomba washirikiane nayo katika kuibua maeneo yenye uharibifu na kuyataja.
Pia, aliahidi kuifanyia kazi changamoto ya ukosefu wa hospitali ya wilaya na kuwataka wananchi kuwa na subira wakati suala hilo likifanyiwa kazi na kwamba, Ilani ya Chama inaelekeza kila wilaya kuwa na hospitali yake.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment