Friday, 4 March 2016

WATAKAOWAKATISHA MASOMO WATOTO WA KIKE KUKIONA-MAJALIWA



SERIKALI imeuagiza uongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha unasimamia kikamilifu elimu kwa watoto wote, hasa wa kike na kuwachukulia hatua wote watakaosababisha kukatisha masomo yao.
Pia, imesema watoto kuanzia umri wa miaka minne hadi mitano wanaandishwa katika madarasa ya awali, ambako ndiko watakakotoka wanafunzi wa darasa la kwanza.
Hayo alisemwa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozumgumza na wananchi wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
"Atakayekwamisha elimu kwa mtoto wa kike atafute mbereko ya kuibebea serikali kwani imejipanga katika kusimamia hilo. Tunataka binti akifaulu kwenda kidato cha kwanza, asizuiwe, asome na viongozi wa serikali simamieni hili," alisisitiza.
Pia, alisema watoto kuanzia darasa la awali watakuwa wanasoma masomo ya kujifunza kuandika, kusoma na kuhesabu ili watakapofika darasa la tatu, wawe na uelewa wa kutosha na kuweza kusoma masomo mengine.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajiwa kuajiri walimu zaidi ya  40,000 ili kumaliza changamoto ya upungufu wa walimu katika shule za msingi na sekondari nchini.
Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na changamoto ya upungufu wa walimu pamoja na vitabu vya kufundishia na kujisomea.

No comments:

Post a Comment