Friday, 4 March 2016
SERIKALI YAWAWEKA MTEGONI WAKUU WA MIKOA NA WILAYA
SERIKALI imewataka wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi, ambao shule zao zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madawati, kujitathmini wenyewe.
Imesema viongozi hao wanaweza kumaliza tatizo hilo kwa kutenga fedha kutoka kwenye vyanzo vya ndani vya mapato na kuwafanya watoto wasome katika mazingira mazuri.
Hayo yalisemwa juzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya kupokea taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Eraston Mbwilo, ambaye aliiomba serikali kuwasaidia katika kutatua tatizo la upungufu wa madawati.
Majaliwa alisema wilaya na mikoa ziweke mikakati na kutenga fedha kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa madawati na kwamba, Rais Dk. John Magufuli, alishatoa maelekezo na kuwataka viongozi watakaokosa madawati katika shule zao wajipime.
Katika taarifa yake, Mbwilo alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ni pamoja na upungufu wa miundombinu kama vile madawati, nyumba za walimu, maabara na vyumba vya madarasa.
Alisema katika shule za sekondari, kuna mahitaji ya madawati 56,487 na yaliyoko ni 39,880, hivyo wana upungufu wa madawati 16,607, ambapo kwa upande wa shule za msingi, zinahitaji madawati 123,087 na yaliyoko ni 51,458, hivyo kuna upungufu wa madawati 71,629.
Mkuu wa mkoa alisema wamejipanga kukabiliana na changamoto hiyo kwa kununua mbao kutoka katika mashamba makubwa ya mbao, ili kuhakikisha kila wilaya inakamilisha utengenezaji wa madawati ifikapo Juni, mwaka huu.
Aidha, alisema mkoa umezielekeza halmashauri zote kufanya matengenezo ya madawati yaliyoharibika katika kila shule na kuwashirikisha wadau wa maendeleo kuchangia upatikanaji wa madawati.
Mbali na changamoto hiyo ya upungufu wa madawati, Mbwilo alisema matundu ya vyoo yaliyoko katika shule hizo hayatoshelezi, ambapo katika shule za msingi, matundu yaliyoko ni 4,388 huku mahitaji yakiwa ni 13,505.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment