MSONGAMANO katika barabara za Jiji la Dar es Salaam, unadaiwa
kusababisha hasara ya sh. bilioni nne kwa siku na sasa mkakati mpya ni kuzuia
magari yenye uzito wa zaidi ya tani 10 kuingia mjini.
Mkuu wa Mkoa wa huo, Said Mecky Sadiki, alisema hayo jana, wakati
akifunga mkutano wa Bodi ya Barabara na kuongeza kuwa, fedha hizo hupotea
kutokana na wananchi kukaa kwenye msongamano, ambapo hukwamisha uzalishaji mali
na kupunguza tija.
Alisema hali hiyo inatokana na jiji hilo kuwa na mtandao finyu
wa barabara uliopo, ikilinganishwa na
idadi kubwa ya magari na vyombo vingine vya usafiri na kwamba, jitihada
zinaendelea ili kumaliza tatizo hilo.
“Ndiyo maana Rais Dk. John Magufuli, kwa kuliona hilo alitoa
sh. bilioni nne kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Ali Hasan Mwinyi kutoka
Morocco hadi Mwenge. Fedha hizo ni zile ambazo zilikuwa zitumike kwa ajili ya
sherehe za Uhuru mwaka jana. Tunamshukuru rais na ujenzi unaendelea vizuri,”
alisema Sadiki.
Ameziagiza manispaa za jiji hilo kuweka
alama za barabarani zinazoonyesha zuio kwa magari yote yenye uzito wa zaidi ya
tani 10, kupita kwenye barabara za lami katikati ya jiji ili wamiliki na
madereva watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Alisema manispaa hizo zinatenga fedha
nyingi za kujenga barabara mpya na kufanya matengenezo ya zile zilizopo, ambazo
nyingi zinaharibiwa na malori ya mizigo.
Alifafanua kuwa matumizi hayo mabaya ya
barabara kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na ukiukwaji wa sheria za barabarani,
ambapo malori makubwa ya mizigo huegeshwa na kuziba maeneo ya waenda kwa miguu,
jambo linalowanyima haki wananchi kutumia maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao.
No comments:
Post a Comment