WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kazi inayofanywa na
serikali ya kuwashughulikia wakwepa kodi, wala rushwa na mafisadi, haitasimama
kamwe, itaendelea hadi kieleweke na hakuna mtu atakayeonewa.
Kufuatia hatua hiyo, Majaliwa amewaomba wananchi kila mmoja
kwa imani yake, awaombee viongozi hao kwa sababu vita wanayopambana nayo ni
kubwa.
Majaliwa, aliyasema hayo juzi jioni, alipozungumza na wananchi
wa wilaya ya Busega, katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye mji wa
Lamadi na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Alisema kazi hiyo ya kuwabana mafisadi, wala rushwa na wakwepa
kodi itakuwa endelevu, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na
rasilimali za taifa, hivyo aliwataka watumishi wa umma watakaoshindwa
kuwajibika ipasavyo, wajiondoe mapema.
Aliongeza kuwa kazi waliyonayo kwa sasa ni kujenga mazingira
ili kila mtu aweze kunufaika na rasilimali za taifa, hivyo aliwataka wananchi
kuhakikisha wanashirikiana na serikali kwa kutoa taarifa za maeneo yote yenye
uharibifu ili yashughulikiwe.
"Kwa mwendo huu Tanzania inaweza kujitegemea kwa asilimia
80, ya bajeti yake na kuondokana na kuwa ombaomba, jambo hili linawezekana
kupitia vyanzo vya ndani na tumeanza kwa kuangalia vyanzo vya mapato na
tunaomba wananchi watuunge mkono,"alisema.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha inakuwa na mapato ya
kutosha kuweza kujiendesha na kwamba, watalazimika kuomba msaada pale itakapobidi,
lakini wanaamini kwamba, kwa kutumia vizuri rasilimali zilizoko, wataweza
kujikwamua na kuondokana na utegemezi.
Majaliwa alisema mapato yanayopatikana katika bandari
yakisimamiwa ipasavyo, yanaweza kulisaidia taifa kupiga hatua kubwa kimaendeleo,
iwapo watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia watakuwa waadilifu.
Katika hatua nyingine, baada ya kuridhishwa na utendaji kazi
wa Waziri Mkuu, hasa katika utumbuaji wa majipu, wazee wa wilaya ya Busega walimtawadha
kuwa kijana wao, ambapo walimpa jina jipya la Masanja na kumkabidhi vitendea
kazi, ikiwemo mkuki kwa ajili ya kutumbulia majipu.
Anusa ufisadi askari wa
hifadhiKatika hatua nyingine, Majaliwa amewataka askari wa wanyamapori kuacha tabia ya kuwahujumu wafugaji na kuwafanya kitega uchumi, kwa kuwashawishi kuingiza mifugo hifadhini kisha kuwazunguka na kuwakamata kwa madai ya kuvamia hifadhi na kuwatoza kati ya sh. milioni tano hadi 10.
Amewaagiza askari hao kuacha tabia hiyo na atakayekamatwa anamuhujumu mfugaji, atachukuliwa hatua kwa kuwa serikali haitakuwa tayari kuvumilia vitendo hivyo.
Majaliwa aliwataka wafugaji watakaotozwa fedha na askari wa wanyamapori, kutoa taarifa kwenye vyombo husika, ambapo pia aliwataka kutoingiza mifugo yao katika maeneo hayo.
Alikuwa akizungumza na wananchi katika eneo la Dutwa, wilayani Bariadi, baada ya wananchi hao kulalamikia kitendo cha askari wa wanyamapori kuwatoza fedha na kukamata mifugo yao.
"Askari wa wanyamapori wanawaita wafugaji na kuwaruhusu kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi na kisha wanawaambia askari weingine, wanakwenda kuwakamata na kudai malipo, jambo ambalo halikubaliki na ni sawa na kuwahujumu wafugaji," alisema.
Awali, Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge, alimuomba Majaliwa kuwasaidia kuhakiki mpaka wa jimbo hilo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa kuwa wananchi wanaonewa na kunyanyaswa na askari wa wanyamapori, ambao hukamata mifugo yao kwa madai kuwa wanavamia maeneo ya hifadhi.
No comments:
Post a Comment