Friday, 15 July 2016
VYETI VYA WATUMISHI WA SERIKALI SASA KUHAKIKIWA UPYA
SERIKALI imeombwa kufanya oparesheni maalumu ya ukaguzi wa vyeti vya watumishi wake ili kukabiliana na ongezeko la matumizi ya vyeti bandia.
Aidha, watendaji wametakiwa kupunguza urasimu katika utoaji huduma, hali inayosababisha kuongezeka kwa wizi wa nyaraka za serikali.
Akizungumza jana, Dar es Salaam, Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Kassian Chibogoyo, alisema hivi karibuni kwa kushirikiana na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamefanikiwa kukamata nyaraka mbalimbali za serikali, jambo linalofanya mahitaji ya operesheni hiyo kuwa makubwa zaidi.
Alizitaja baadhi ya nyaraka walizozikamata kuwa ni pamoja na vyeti vya ukazi, kuzalisha, stakabadhi za mapato, leseni za biashara, vibali vya serikali, shahada za ndoa kutoka Kanisa Katoliki la Mtakatifu Maria Magomeni na maboksi matatu ya kadi za bima za magari.
Alisema pia wamekamata vyeti vya elimu ya sekondari na vyuo vikuu, ikiwemo kutoka Chuo Kikuu cha Kampala na kadi za uraia, vyote vikiwa vya kughushi.
“Hali hii inatia wasiwasi kwamba huenda hata wataalamu wengi tulionao wanatumia vyeti hivyo.
"Kutokana na hali hii, ipo haja kufanyika msako mkali wa vyeti vya watumishi na ofisi yangu haitaogopa mtu. Tumejipanga kupigania nchi na tutashinda kukabiliana na uhalifu hatari wa nyaraka za serikali,"alisema.
Chibogoyo alisema uhalifu huo ni hatari kwa usalama wa nchi na mali zake kuliko ujambazi kwa kuwa hivi sasa, inaonekana kuna soko kubwa la nyaraka hizo kutoka mtamboni.
Alisema hatua ya kudhibiti matumizi ya nyaraka hizo itasaidia kulinda mipaka ya nchi na zikiachwa zitumike, zitasababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo kwa kuwa serikali ikiwa haina mapato, watu wananufaika kwa kutumia leseni za biashara na stakabadhi za mapato feki.
Alisema ipo haja jamii kupewa elimu ya sheria kuhusu uhalifu huo kwa kuwa katika sheria mbalimbali, ikiwemo sheria ya ushahidi, sheria ya usalama wa taifa, sheria ya kudhibiti nembo na ngao ya taifa, inaonya na kuelekeza adhabu, ikiwemo kifungo cha miaka saba kwa mtu atakayejihusisha.
"Mtandao huo ni vyema kuacha kabisa kuhujumu nyaraka za serikali. Tunajua sehemu zote za mauzo na tupo katika oparesheni ya okoa pato la taifa, tutawafikia wote,"alisema.
Chibogoyo alisema hatua hiyo itafanikiwa kwa kuwa utengenezaji nyaraka bandia ni hatari, hasa katika matumizi ya taasisi nyeti, ikiwemo udaktari, mahakama, ualimu na huduma zingine.
Alisema vita ya kupambana na wachapishaji wa nyaraka bandia kwa sasa haitakuwa na suluhu kwa kuwa waathirika wakubwa ni Watanzania wote.
Alisisitiza haja ya watumishi wa serikali, ikiwemo ofisi za serikali za mitaa kupunguza urasimu katika kutoa huduma ili watu kupata baadhi ya nyaraka kwa urahisi, hatua itakayomaliza biashara ya nyaraka feki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment