MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Maonda, ametangaza
rasmi kuanza msako mkali wa nyumba kwa nyumba ili kubaini shughuli za kila
mkazi mkoani humo.
Aidha, amesema ataliagiza Jeshi la Polisi na Kuiomba
Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kuwachunguza na
kuwakamata viongozi wa serikali za mitaa
na yeyote, ambaye atathubutu kuzuia au kukataa kutoa ushirikiano kwa maofisa
watakaoendesha sensa hiyo.
Makonda alisema hayo jana, wakati akipokea madawati 30, yaliyotolewa na Serikali ya Mtaa wa
Karume, Kata ya Ilala, Dar es Salaam.
Alisema ameshaanza vikao na wakuu wa wilaya zote tano za mkoa huo, ambazo ni Ilala, Kinondoni,
Temeke, Ubungo na Kigamboni, ili
kukamilisha mpango huo, aliosema
utaanza muda wowote kutoka sasa.
“Tunaanza operesheni yetu rasmi ya nyumba kwa nyumba ili kubaini kila shughuli anayofanya mkazi wa Dar es Salaam.
Tunataka kuwasaidia watu. Kuna watu wanakaa katika nyumba za watu bila shughuli
maalumu. Makonda anataka kuwasaidia,”alisema
mkuu huyo wa mkoa.
Aliongeza: “Usikae kwenye nyumba ya mtu kama huna
jukumu. Wengine wanapewa mitaji, wanakula halafu wanarudi kuwa mizigo. Ni
lazima kila mmoja afanye kazi na tutaandika.”
Alisema amepata taarifa za kuwepo kwa baadhi ya watu,
ambao hawatoi ushirikiano kwa viongozi wa serikali za mitaa wanaofanyakazi ya kuorodhesha kila shughuli
katika kaya.
“Si muda mrefu nitaelekeza Jeshi la Polisi na TAKUKURU
kuwachunguza na kuwakamata kwa sababu mtu anayezuia serikali kujua shughuli za watu anaoishi nao,
ni lazima mtu huyo atakuwa na nia mbaya.
Ni lazima atakuwa anauza dawa za kulevya, ana danguro, anajihusisha na magendo au biashara ya
binadamu,”alisema Makonda.
“Haiwezekani
ukamzua mwenyekiti wa serikali ya mtaa kujua watu unaoishi nao katika nyumba yako wakati huyo ndiye mwenyekiti wa
kamati ya ulinzi na usalama katika mtaa. Haiwezekani,” alisisitiza.
Alisema operesheni hiyo itakuwa kubwa na itakuwa
ikifanyika usiku na mchana, kwa sababu baadhi ya watu wanapatikana mchana na
wengine huonekana usiku.
“Ni lazima tujue kila mtu anafanya nini ili wale ambao hawana shughuli maalumu, tujue
namna ya kuwasaidia. Haiwezekani mtu ukaishi bila shughuli yoyote ya
kujiingizia kipato. Nitafuatilia, nitasimamia hadi tuhakikishe operesheni hiyo
inafanikiwa,”alisema.
Makonda aliupongeza uongozi wa serikali ya mtaa wa
Karume kwa kuwa mtaa wa kwanza nchini
kuchangia madawati.
“Mtaa huu umeandika historia. Tokea tumeanza zoezi la
kuchangisha madawati, mtaa huu wa Karume ndiyo wa kwanza kuchangia,”alisema.
Akikabidhi madawati hayo, Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Haji
Bechina, alisema wameamua kutoa mchango huo ili kuunga mkono jitihada za Rais Dk. John Magufuli na mkuu huyo
wa mkoa.
“Tunatambua jitihada za serikali yetu na juhudi zako
binafsi kama mkuu wa mkoa katika kutatua changamoto ya uhaba wa madawati,”alisema Bechina.
Diwani wa Kata ya Ilala Sad Kimji, alisema wanajisikia fahari kutoa madawati hayo kwa
sababu ofisi ya mkoa wa Dar es Salaam, iko ndani ya kata hiyo.
No comments:
Post a Comment