Friday 15 July 2016

OMBO LA TUNDU LISSU LATUPWA MAHAKAMANI


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imesema ina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) na wahariri wa gazeti lililofungiwa kwa muda usiojulikana la Mawio.

Kutokana na hilo, mahakama hiyo imetupilia mbali pingamizi lililokuwa limewasilishwa na wakili wa washitakiwa hao, Peter Kibatala la kwamba haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, ambayo inahusisha Zanzibar.

Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote husika, mahakama hiyo imeona kwamba ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

“Mahakama hii ina mamlaka ya kusikiliza kesi hii mpaka mwisho. Kwa msingi huo, pingamizi la utetezi linatupwa kwa kuwa halina msingi kisheria,"  alisema Hakimu Simba na kuahirisha shauri hilo hadi Agosti 2, mwaka huu.

Mbali na Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni wahariri wa gazeti la Mawio, ambalo linadaiwa kuchapisha habari ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘Machafuko yaja Zanzibar’, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu, ambayo ni kuchapisha taarifa za uchochezi na kuchapisha gazeti bila kuwasilisha hati ya  sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, Januari 14, mwaka huu, katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam.

Baada ya washitakiwa hao kusomewa mashitaka hayo, wakili Kibatala aliwasilisha hoja kupinga baadhi ya mashitaka, akidai hayapo sahihi mahakamani hapo kwa kuwa hayajapata kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Pia, Kibatala aliiomba mahakama hiyo kuiondosha hati ya mashitaka kwa  sababu hayajakidhi matakwa ya  sheria.

Kibatala alidai mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa Sheria ya Magazeti sio miongoni mwa masuala yaliyoko katika Muungano.

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, alikiri mashitaka mawili kufunguliwa bila ya uwepo wa kibali cha DPP, hivyo aliamua kuyaondoa.

Kadushi alidai madai mengine ya utetezi hayana msingi na kwamba mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

No comments:

Post a Comment