WATU 10 wakiwemo ndugu wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na tuhuma za kujihusisha na nyara
za serikali na kukutwa na vipande 660 vya meno ya tembo vyenye thamani ya sh.
bilioni 4.5.
Washitakiwa hao wakiwemo raia wawili wa Guinea,
walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa polisi na kupandishwa
kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk. Yohana Yongolo.
Raia hao wa Guinea ni wafanyabiashara Ally Sharif (28)
na Fatoumata Saumaolo (24).
Washitakiwa wengine ni mfanyabiashara Victor Mawalla
(29), mwanafunzi Calisti Mawalla (22), wafanyabiashara Haruna Kassa (37), Abbas Hassan au Jabu (40),
mkulima Solomon Mtenya (46) na dereva Mussa Ligagabile (59).
Pia, wamo Khalfan Kahengele (64) na Ismail Kassa (53),
wote wakazi wa Dar es Salaam.
Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kwa kushirikiana
na Mawakili wa Serikali, Simon Wankyo, Salim Msemo na Paul Kadushi, waliwasomea
washitakiwa hao mashitaka matatu yanayowakabili.
Mawakili hao waliwasomea washitakiwa hao mashitaka ya
kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kujihusisha na nyara za serikali na
kupatikana na vipande hivyo vya meno ya tembo, vyenye thamani ya sh.
4,570,347,951, mali ya serikali bila ya kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa
Wanyamapori.
Wakiwasomea mashitaka hayo, washitakiwa wote wanadaiwa
walitenda kosa hilo, tarehe tofauti kati ya Aprili 6 na Juni 23, mwaka huu,
ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam.
Inadaiwa walipanga, waliratibu, kusimamia na kufadhili
vitendo vya mtandao wa kihalifu kwa kununua, kupokea na kusafirisha nyara za
serikali, ambazo ni vipande 666 vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Dola za
Marekani 2,105,181 (sawa
na sh. 4,570,347,951), mali ya serikali bila ya kuwa na
kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia, washitakiwa hao wote wanadaiwa katika kipindi
hicho, mkoani Dar es Salaam, kwa pamoja walinunua, kupokea na kusafirisha
vipande hivyo vya meno ya tembo vyenye thamani hiyo.
Washitakiwa Sharif, Victor, Calisti, Kassa na Jabu
wanadaiwa Juni 23, mwaka huu, maeneo ya Mbezi Msakuzi, wilayani Kinondoni, Dar
es Salaam, walikutwa na nyara za serikali, ambazo ni vipande hivyo vya meno ya
tembo, bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Dk. Yongolo
aliwataarifu washitakiwa kwamba hawapaswi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo
haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Upande wa jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na
kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Washitakiwa hao wanaotetewa na mawakili Hamza Jabir, Aloyce Komba na
Barnabas Lugua, walirudishwa rumande hadi Julai 28, mwaka huu, kesi itakapokuja
kwa kutajwa.
Washitakiwa hao, ambao waliondolewa mahakamani hapo
kupelekwa mahabusu chini ya ulinzi mkali wa askari, walikamatwa na Kikosi Kazi
cha (Task Force) ya Taifa.
No comments:
Post a Comment