WAZIRI MKUU Kasim Majaliwa amesema serikali itahakikisha inaunga mkono dini zote nchini na kuzipa ushirikiano wa kutosha ili ziweze kufanya kazi zake vizuri.
Waziri Mkuu aMajaliwa alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Malolo na Chimbila ‘B’ akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi ya siku tatu kukagua shughuli za maendeleo wilayani Ruangwa, Lindi.
“Dini ndiyo inayojenga msingi imara kiroho, kiimani na ndiyo inayojenga maadili mema. Leo tunaposema kila mtu awe muadilifu tumegundua ili tufanikiwe lazima tuweke mazingira mazuri yatakayowezesha madhehebu yote kuabudu kwa uhuru,”alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli imegundua kwamba ili iweze kufanikiwa ni lazima ishirikiane na madhehebu yote ya dini ili kufanikisha mipango mbalimbali.
“Nikiwa mtendaji mkuu wa shughuli za serikali niliamua kuunda Kamati ya Amani ya Taifa ambayo inajumuisha viongozi wa dini zote. Pia, nimeiagiza mikoa na wilaya zote kuunda kamati za amani ili kuhakikisha umoja na maelewano miongoni mwa dini zote nchini unakuwepo,” alisema.
Alisema lengo la kamati hizo ni kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na maadili mema na kutambua umuhimu wa kuimarisha amani na utulivu nchini.
Akizungumzia tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vya Nanganga, Nangumbu, Mbecha, Malolo, Mpumbe na Chimbila ‘B’ alisema serikali inalifanyia kazi suala hilo.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema tayari mtaalamu wa kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi ameshawasili katika wilaya hiyo na baada ya kukamilisha utafiti huo shughuli ya uchimbaji visima itaanza.
Kwa mujibu wa Majaliwa, lengo la utafiti huo ni kutaka kubaini wingi na ubora wa maji katika eneo husika hivyo aliwataka wananchi kwenye vijiji husika kuwa na subira wakati suala hilo likishughulikiwa.
No comments:
Post a Comment