Saturday 27 August 2016

JPM: VITA DHIDI YA RUSHWA NI ENDELEVU

RAIS Dk. John Magufuli amesema serikali imeweka kipaumbele katika uwajibikaji na kupambana na rushwa huku ikiongeza kasi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha pato la taifa linakuwa.

Dk. Magufuli alisema hayo jana, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, wakati wa ufungaji wa mkutano wa siku mbili wa Diaspora, uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort.

Alisema mikakati ya serikali ni kufikia malengo ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, katika sekta ya viwanda, uwekezaji, kilimo na utalii na kusaidia kukua kwa pato la taifa.

Rais Dk. Magufuli aliwaambia wana diaspora kwamba, serikali ipo katika mikakati ya kukuza uchumi na sekta ya uwekezaji pamoja na uwajibikaji na kupambana na rushwa ili kuwepo mafanikio katika sehemu za kazi.

Alitoa mfano kuwa pato la taifa linaendelea kukua kutoka asilimia 7.0, katika mwaka 2015 na kufikia asilimia 7.2, katika mwaka 2016, ambapo uchumi umekuwa kwa pato la taifa kufikia asilimia 7.0, sawa na kiwango cha ukuaji cha mwaka 2014.

Alisema hatua hiyo imesababisha mfumuko wa bei wa taifa kwa sasa kufikia asilimia 5.1, hatua ambayo imeonyesha kuwa kiwango cha kupanda bei kwa bidhaa mbalimbali kimepungua na kutoa unafuu mkubwa kwa wananchi kupungua kwa ukali wa maisha.

"Hayo ni sehemu ya mafanikio katika kipindi kifupi cha uongozi wangu. Nimedhamiria kukusanya kodi, kupunguza rushwa na kupambana na ufisadi katika sehemu za kazi na uwajibikaji ili kuweka nidhamu inayotakiwa serikalini," alisisitiza Rais Dk. Magufuli.

Pia, ameagiza Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuharakisha mchakato wa kuwepo kwa sera ya diaspora ili kuifanya jamii hiyo kutoa mchango wake kikamilifu wa uchumi wa taifa.

Alisema kuwepo kwa sera ya diaspora itakuwa muongozo kwa ajili ya kuwawezesha na kuwashirikisha kikamilifu katika mchango wa taifa na kukuza pato la taifa.

Akizungumzia suala la uraia pacha, Rais Dk. Magufuli alisema ni muhimu kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo kwa Watanzania waliopo ughaibuni na kuchangia maendeleo kikamilifu.

Alisema serikali imejizatiti kulishughulikia suala hilo kikamilifu kwa ajili ya kuona mchango wa diaspora unainufaisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Afrika.

"Nipende kuwahakikishia wana diaspora kwamba, serikali yenu imejizatiti kulishughulikia suala hilo kikamilifu, ambapo imani yangu huko mbeleni tutafikia hatua nzuri zaidi," alisema.

Mapema akimkaribisha Rais Dk. Magufuli kuzungumza, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga,  aliwataka wana diaspora kuwa mabalozi wa kisiasa wakati wanapokuwa nje ya nchi na kujenga tabia nzuri ya mahusiano kwa makundi mbalimbali.

Aliwataka kuacha kujishughulisha na matumizi ya dawa za kulevya, ambazo kwa kiasi kikubwa zimeipa sifa mbaya Tanzania katika ramani ya kidiplomasia, ikiwemo Watanzania wengi kuishia magerezani.

Mkutano wa siku mbili wa wana diaspora ulifunguliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, ambaye aliwataka kuzitumia fursa zilizopo nchini kwa ajili ya kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment