Sunday 8 January 2017

MAJALIWA AONYA VITA YA MADIWANI NA WATUMISHI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa idara kwenye halmashauri za wilaya na manispaa, wasaidie kutoa utaalamu ili wafanikishe maendeleo badala ya kupingana na madiwani.

Pia, amewataka madiwani wasikilize ushauri wa kitaalamu unaotolewa na wakuu wa idara katika utekelezaji wa miradi iliyotengwa na halmashauri.

Alitoa wito huo jana, wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mabada, viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma, akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani humo.

“Wakuu wa Idara nyie ni washauri. Tumieni taaluma zenu kutoa ushauri, semeni bila woga pale inapodidi. Ninawasihi waheshimiwa madiwani wasitumie fursa yao ya ‘kuazimia’ pale inapotokea kuna watumishi wenye msimamo,”alisema.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu alisema serikali iko makini kwenye matumizi kwa kila senti inayokusanywa na akawataka watumishi hao kila mmoja aongeze mapato ya serikali kupitia sekta aliyopo.

Aidha, amepiga marufuku matumizi holela ya fedha za umma.

“Kuanzia leo, marufuku kwa fedha iliyokusanywa kwa mapato ya ndani kutumika bila utaratibu. Serikali hii haina mzaha na miradi inayotekelezwa chini ya viwango. Mtumishi ukiharibu hapa Madaba, usidhani utahamishwa, tunamalizana na wewe hapahapa. Wala usiombe ndugu yako akuombee uhamisho, tutakufuata huko huko,”alisisitiza.

Aliwataka watumishi wa umma watumie Ilani ya Uchaguzi ya CCM, katika kutekeleza majukumu kwani inaeleza kila kitu, ambacho serikali inatakiwa kukifanya katika kipindi cha miaka mitano.

“Zaidi ya hayo, ninawasihi kila mkurugenzi atoe nakala ya hotuba ya Rais ambayo aliitoa Novemba 20, 2015, wakati akizindua Bunge la 11, awape watendaji wake waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwani ilitoa dira ya nini anataka kufanya katika serikali hii,”alisema.

Waziri Mkuu alisema serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi na imeanza kulipa madeni yaliyokuwa yamelimbikizwa.

“Serikali imedhamiria kupunguza madeni ya watumishi na hadi kufikia Novemba 30, 2015, shilingi bilioni 28.9 zilikuwa zimekwishalipwa kwa watumishi 31,032, wenye madai katika sekta mbalimbali. Hilo linaendelea,”alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa wilaya hiyo wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali dini, itikadi, kabila au hali zao na kusisitiza kuwa, serikali haitamwonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.

Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja au cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya. 

"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo,"alisema.

No comments:

Post a Comment