Monday 16 January 2017

MTIHANI KIDATO CHA PILI, UFAULU WAONGEZEKA KWA ASILIMIA 93.3


BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA ), limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili na darasa la nne, ambapo wavulana wameendelea kufanya vyema.

Katika matokea hayo, mkoa wa Mtwara umeshika nafasi mwisho kitaifa, baada ya shule tisa kati ya 10, zilizofanya vibaya zaidi kwenye mtihani wa kidato cha pili kutokea mkoani humo.

Akizungumza Dar es Salaam, jana, Katibu Mtendaji wa NECTA,  Dk. Charles Msonde, alisema katika matokeo hayo, ufaulu umeongezeka kwa asilimia 93.3, ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana.

Dk. Msonde alisema  takwimu za matokeo ya upimaji zinaonyesha kuwa, wanafunzi 372,228, sawa na asilimia 91.8, walipata ujuzi wa maarifa ya kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.

Alisema kati ya hao, wasichana ni 189, 161 na  wavulana 183,067, huku wanafunzi 36,737, wakishindwa kupata wastani wa kuwawezesha kuendelea.

“Idadi inaonyesha kuwa watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu ni 178,115, sawa na asilimia 43.55, wasichana wakiwa 78,466, sawa  na asilimia  37,45 na wavulana ni 99,649, sawa na asilimia 49.97,”alisema.

Msonde alizitaja  shule zilizoongoza kwenye mtihani wa kidato cha pili kuwa ni St. Francis Girls (Mbeya), Kilimanjaro Islamic (Kilimanjaro), Kaizirege Junior (Kagera), Canossa (Dar es Salaam), Twibhoki (Mara) na Shule ya Wavulana Tengeru (Arusha).

Alizitaja zingine kuwa Shule ya  Wavulana Marian (Pwani), Precious  Blood (Arusha), Thomas More Machrinas (Dar es Salaam) na Shule ya Wavulana Shamsiye (Dar es Salaam).

Kwa upande wa shule 10, zilizofanya vibaya zaidi alizitaja kuwa ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukokoda zote za mkoani Mtwara ikifuatia Nyelo (Tanga).

Aidha, NECTA imefuta matokeo kwa watahiniwa 31 waliobainika kufanya udanganyifu  katika upimaji wa kitaifa, ambapo wataruhusiwa kurudia mitihani hiyo mwaka huu.

Pia, imezitaka mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wote waliohusika kusababisha kutokea kwa udanganyifu kwenye mitihani hiyo.

“Tathmini za awali zinaonyesha ufaulu wa wanafunzi kwa masomo ya msingi ya Civics, Historia, Jografia, Kiswahili, Kingereza na Baiolojia uko juu ya wastani.

“Kwa masomo ya Hesabu, Fizikia  na Kemia, ufaulu upo chini ya wastani. Kutokana na hilo, juhudi zinahitajika kuweza kuinua kiwango cha ufaulu wa masomo haya,”alisema.

Alisema NECTA itafanya uchambuzi wa kina wa matokeo hayo kwa kila somo na kutoa  machipisho ya uchambuzi, yatakayowasilishwa kwa wadau wa elimu, lengo likiwa  ni kuwawezesha walimu  kutumia taarifa za uchambuzi kuboresha ufundishaji na ujifunzaji  shuleni.

Akitoa taarifa kwa  mtihani wa darasa la nne, Msonde alisema takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa, wanafunzi walifanya vizuri katika masomo ya Stadi za kazi, Haiba na Michezo, ambayo ufaulu wake ni asilimia  94.67, huku somo la Kingereza likiwa na ufaulu kwa kiwango cha chini, sawa na asilimia 72.51.

Msonde alizitaja Halmashauri 10 zilizofanya vizuri kuwa ni Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Halmashauri ya Mji wa Makambako, Tanga mjini,  Chato,  Mafinga Mjini, Mufindi,  Ilala, Biharamulo,  Hai na Muleba.

Kwa upande  wa shule zilizofanya vizuri ni  St. Leo The Great (Tabora), Acacia  Land (Tabora), Kamada (Geita), Waja Springs (Geita), Twibhoki (Mara), Imani (Kilimanjaro),  Msasa( Geita), St. Peter Claver (Kagera), Chalinze Modern Islamic (Pwani) na  Mudio Islamic (Kilimanjaro).

Baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa  58,  waliobainika  kufanya udanganyifu katika upimaji huo,  ambapo  watarudia mitihani yao mwaka huu.

Hata hivyo, NECTA imewataka walimu kuwafuatilia kwa karibu wanafunzi waliopata ufaulu wa chini  ili waimarike na kuweza kupata ufaulu wa juu.

No comments:

Post a Comment