Monday, 16 January 2017

WALEI WAMTAKA ASKOFU MOKIWA AACHIE NGAZI

SAKATA la Askofu Dk. Valentino Mokiwa kutaka kuvuliwa uongozi wa nafasi ya Uaskofu wa Kanisa la Aglikana Dayosisi ya Dar es Saalam, limezidi kuchukua sura mpya baada ya walei wa Dayosisi hiyo kumtaka askofu huyo kuheshimu uamuzi uliotangazwa na mamlaka zilizo juu yake.

Walei hao walitoa tamko hilo jana, Dar es Saalam, wakati wa ibada ya Jumapili, katika Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Dar es Salaam, lililoko Magomeni.

Akitoa tamko hilo, Kiongozi wa Walei hao wa Dayosisi ya Dar es Saalam, Sylvester Haule, alisema wanaunga mkono uamuzi wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Muhashamu Dk. Jacob Chimeledya, kumvua uongozi Dk. Mokiwa.

Alisema uamuzi wa kumvua uaskofu Dk. Mokiwa unapaswa kuheshimiwa kwa kuwa unatoka kwa kiongozi mkuu wa kanisa hilo, hivyo anapaswa kuheshimiwa mamlaka yake ya juu ili wengine waweze kujifunza kutoka kwake.

“Sisi Walei tunawasihi wenzetu Makasisi, Mashemasi na Wainjilisti, ambao wanatumika pasipo kujifahamu na kupoteza utii kwa Baba Askofu Mkuu, wajitafakari kwa kuwa wao bado ni wachungaji wetu wa kiroho, Mungu hawezi kuvumilia kama tutaendelea na roho hii ya kumkosea utii Askofu wetu mkuu, ambaye ni mwangalizi wa kanisa na kumtii aliyevuliwa madaraka,”alifafanua.

Haule aliongeza kuwa, kama kuna baadhi ya watu wanaona Askofu Mokiwa anaonewa kwenye suala hili, ni vizuri wakapata wasaa wa kutembelea maeneo yanayolalamikiwa kufanyika uwekezaji usio na manufaa kwa kanisa.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na shamba la kanisa hilo lililoko Mtoni Buza, nyumba ya Askofu iliyoko Oysterbay, jengo la Kanisa la Silver Oak, Kanisa la Mtakatifu Andrea Magomeni, Kanisa la Mtakatifu Mariamu Kurasini, eneo la Kanisa Buguruni Malapa na kwingineko.

Mbali na hilo, kiongozi huyo alitolea ufafanuzi madai ya kutumika kwa fedha zilizotolewa na wawekezaji, ambapo alidai nakala ya benki (Benki Statement) kutoka Benki ya Akiba, ambayo ilifunguliwa katika akaunti ya Uinjilisti (Diocese of Dar Es Salaam Evangelism, AC: 10200561029), inaonesha sh. 1,392,000,000 ziliingizwa kwa nyakati tofauti na kutumika kwa maanufaa binafsi kwa muda mfupi.

“Askofu Dk. Mokiwa anajua undani wa matumizi ya fedha hizo zilizoko kwenye akaunti hiyo, ambayo kwenye vitabu vya hesabu za Dayosisi yetu haikutunzwa taarifa zake mahala popote. Fedha zote zilizotokana na uwekezaji ndani ya Dayosisi zingeweza kusaidia shughuli nyingi za maendeleo na huduma, ikiwemo kuwagharimia wahudumu,”alisema.

Haule alisema baadhi ya wahudumu ndani ya Dayosisi hiyo walipewa maeneo, ikiwemo Mtoni Buza ili wajenge kwa ajili ya kuishi, lakini badala yake wengine walikodisha kwa wawekezaji na wanalipwa fedha nyingi.

“Waumini tumekuwa na mzigo mkubwa wa kuhudumia Dayosisi kama mipango ingekuwa mizuri na inatekelezwa pasipo viongozi kutanguliza maslahi yao binafsi. Mzigo wa kuhudumia kanisa ungepungua kwa kuwa vitega uchumi vya Dayosisi vingetumika kusaidia kazi za kanisa ikiwemo kulipa wahudumu,”alisema.

Alisema kitendo cha Askofu Dk. Mokiwa kupingana na uamuzi wa kuvuliwa uongozi wake ni utovu wa nidhamu na viapo vya utii.

Januari 7, mwaka huu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Muhashamu Dk. Jacob Chimeledya, aliamuru aliyekuwa Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Mokiwa, kujiuzulu na kustaafu nafasi hiyo baada ya kubainika alihusika kwenye vitendo vya ubadhirifu wa mali za kanisa.

Wakati huo huo, makanisa ya Mbezi, Ubungo, Yombo, Buza, Malamba mawili na Kurasini, yamepanga kugomea uongozi wa Dk. Mokiwa.

Uamuzi wa kumvua wadhifa Dk. Mokiwa, ulichukuliwa baada ya Machi 3, mwaka 2015, walei 32 kutoka makanisa mbalimbali ya dayosisi hiyo, kuwasilisha mashitaka wakidai kuwepo na tuhuma za ukosefu wa maadili na kutaka Askofu Dk. Mokiwa, anyang’anywe madaraka hayo.

Walei hao waliwasilisha mashitaka 10, dhidi ya Dk. Mokiwa, yakiwemo kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa kwenye eneo la Kanisa la Mtoni Buza, kinyume na kifungu cha 29 cha Katiba ya Dayosisi na kanisa hilo.

Mashitaka mengine ni pamoja na kudaiwa kufunguliwa mashitaka mahakamani na Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, Erasto Mhagama, Christopher Njavike na George Mwafalo kwa kosa la kuwatishia kwa silaha ya moto.

Pia, Askofu Dk. Mokiwa alidaiwa kutoa Daraja la Ushemasi, Upadre na Ucanon kwa Katibu wa Dayosisi, ambaye alitengana na mkewe kisha kuoa mke mwingine kiserikali, kitendo ambacho ni kinyume na kanuni VII (1) ya kanuni ya ndoa.

No comments:

Post a Comment