UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umewataka Watanzania kuwapuuza Waziri Mkuu mstaafu, Feredrick Sumaye na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowasa kwa kuwa wanaota ndoto za mchana.
Umesema kuiombea CCM kushindwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ni sawa na kujifisha akili za abunuasi, ambaye siku zote mipango yake haitimii.
Aidha, umoja huo umesema upinzani wa Tanzania haukubaliki mbele ya wananchi wazalendo na hata wapigakura hawatakuwa tayari kuvipa ridhaa vyama, ambavyo baadhi ya viongozi na wagombea wake ni waumini wa ufisadi na sio wachapakazi.
Msimamo huo ulitolewa jana, mjini hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipohutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro mjini hapa.
Shaka alisema wananchi hawana budi kumpuuza Sumaye, Lowasa na chama chao cha CHADEMA, kwa sababu sio viongozi wenye uadilifu bali ni wasaka madaraka walio na pupa na uroho wa uongozi wa juu wa nchi wakati hawana sifa ya kupewa nafasi hiyo.
Alisema Watanzania wana shida ya kupata maendeleo ya kisekta na maisha bora na kamwe hawatamani maneno matupu, propaganda uchwara kama zinazofanywa na Sumaye, Lowasa na wenzao.
"Watanzania wapuuzeni watu hawa kwa sababu Sumaye ni Pwagu na mwenzake Lowasa ni Pwaguzi, wanahaha usiku na mchana kusaka madaraka wakati wananchi wanawajua sio waadilifu na hawaaminiki katika jamii,"alisema.
Alisema kutokana na utendaji wa serikali ya awamu ya tano unaothamini haki na maslahi ya wananchi wanyonge, CCM tayari imeshajihakikishia ushindi kabla ya mwaka 2020.
Kaimu Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha wananchi kuwa, Sumaye ndiye aliyekuwa kinara, akisema ikiwa CCM itamsimamisha Lowasa kuwa mgombea urais, atahama na Chama, lakini ilipoyakata majina yao, aliyakana maneno yake na kuhama CCM kwenda kumfuata Lowassa, aliyetangulia CHADEMA kusaka vyeo na madaraka.
"Wapinzani wanahofia kasi ya utendaji wa serikali ya Rais Dk. John Magufuli, wanajua wameporwa hoja za kuwaeleza wananchi kwa sababu kero na matatizo yote yaliyokuwa yakilalamikiwa sasa yanatatuliwa na serikali ya awamu ya tano,"alisema.
Akimnadi mgombea wa CCM katika uchaguzi huo, Shaka aliwaomba wananchi kumchagua Sengo Mtandikile, kwa kuwa ni mchapakazi, mahiri, hodari na anayependa kushirikiana na wananchi.
Shaka alisema CCM imeamua kumsimamisha Sengo kuwa mgombea baada ya kumpima na kujiridhisha ana vigezo vya kutosha na kuonekana anafaa kuwawakilisha wananchi wa kata hiyo katika Manispaa ya Morogoro kwa nafasi ya udiwani.
Kwa upande wake, Sengo aliwahakikishia wananchi wa Kiwanja cha Ndege kwamba, akishinda uchaguzi huo atajikita katika kuwatumikia ili kukuza maendeleo ya kisekta kama ilivyoahidiwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya Morogoro Mjini, Fikiri Juma na Kaimu Katibu wa Mkoa wa Morogoro, Kurwa Milonge.
No comments:
Post a Comment