Monday, 16 January 2017

WATOTO WA MAOFISA WA MAGEREZA WAFIA KWENYE GARI


WATOTO wawili wa maofisa wa Jeshi la Magereza, wamefariki dunia baada ya kujifungia kwenye gari la mmoja wa wazazi wao, walipokuwa wakicheza na hatimaye kukosa hewa.

Tukio hilo lilitokea juzi, jioni, katika kota za Magereza Ukonga, wakati wazazi wao wakitengeneza gari hilo.

Watoto hao waliokufa ni mtoto wa Mrakibu wa Jeshi la Magereza (ASP), Demetrus Masala, aitwaye Mariam (6), aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya St. Theresa, Ukonga na Esther (4), mtoto wa Sajini Francis, aliyekuwa akisoma shule ya awali.

Mashuhuda wa tukio hilo, ambao hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, walidai watoto hao walipoteza maisha katika gari lenye namba T 291 CXR  aina ya Toyota Passo, mali ya ASP Masala.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio, gari hilo liligoma kuwaka ndipo Masala alipokwenda kumuomba jirani yake, ambaye anaishi mlango wa pili, Francis aje amsaidie kuliwasha.

Francis, ambaye ni dereva wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu, walishirikiana na Masala kuliwasha gari hilo kwa muda mrefu, lakini
ilishindikana kuwaka.

Wakati wazazi hao wakiendelea kulitengeneza gari hilo, ndipo watoto hao waliposogelea, ambapo licha ya kuwafukuza,  waliingia garini bila wazazi wao kufahamu kwa sababu lilikuwa na vioo vya giza.

Baada ya kushindikana kuwaka, ndipo Francis alipomwelekeza mwenzake kwa fundi, ambaye angeweza kulitengeneza.

“Kutokana na ushauri huo, Masala aliamua kulifunga gari lake na kuondoka kumfuata fundi bila kufahamu kama watoto hao wameingia ndani ya gari hilo,” kilieleza chanzo hicho.

Mmoja wa mashuhuda hao alidai kuwa, baada ya kukaa kwa muda mrefu, Francis alibaini watoto hao wawili hawaonekani maeneo hayo na kuanza kuwatafuta bila mafanikio.

Inadaiwa wakati wakiendelea kuwatafuta, kuna kijana akawadokezea kuwa wakati gari hilo likiendelea kutengenezwa, watoto hao walikuwa ndani ya gari hilo.

Kauli hiyo inadaiwa ndiyo iliyomshtua Francis na kuamua kuchungulia ndani ya gari hilo, ambapo walibaini watoto hao wakiwa wamekaa siti ya nyuma wamelala fofofo huku mwingine akivuja damu puani.

Hali hiyo ilisababisha Francis na wengine waliokuwepo eneo hilo kusogea na kuvunja kioo cha gari hilo na kuwatoa watoto hao wakiwa katika hali mbaya.

Imedaiwa kuwa kutokana na hali za watoto hao kuwa mbaya, waliamua kuwakimbiza katika Hospitali ya Kardinal Rugambwa, Ukonga kwa ajili ya matibabu ya haraka, lakini ikabainika kuwa mtoto Mariam tayari alikuwa amekwishafariki.

Madaktari walijaribu kuokoa maisha ya mtoto Esther kwa kumuongezea hewa ya oksijeni na baadaye kumkimbiza Hospitali ya Amana, ambako ilibainika amefariki dunia.

Imedaiwa kuwa wazazi wa watoto hao kila mmoja alikuwa na watoto wawili wa kwanza wote wa kiume na wa pili wa kike, ambao ndio waliofariki katika tukio hilo.

Mwili wa mtoto Mariam ulisafirishwa jana kwenda mkoani Rukwa kwa mazishi.

Familia ya Francis inatarajia kufanya mazishi ya mtoto wao Esther kesho katika makaburi ya Segerea, Ukonga.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu, Deus Nchimbi alisema kifo cha watoto hao ni pigo kwa familia hizo marafiki.

“Kikubwa ni kuomba amani na kuwaombea marehemu, lakini watoto wamekufa kifo cha uchungu kwa kukosa hewa. Huenda wangekuwa na wakubwa, wangeweza kufungua gari,”alisema Nchimbi.

Alisema kilichobaki ni kuikumbusha jamii kuwa makini na vyombo vya moto.

No comments:

Post a Comment