Monday 16 January 2017

NCHI HAINA NJAA- MAJALIWA


SERIKALI imesema nchi haijakumbwa na baa la njaa na kuwataka wananchi kutosikiliza kampeni za upotoshwaji zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiasha kuhusu hali ya chakula kwani sio za kweli, bali ni za uzushi na zenye lengo la  kupandisha bei za vyakula.

Imesema kelele za uzushi zinazotolewa kuhusiana na kuwepo kwa baa la njaa nchini, hazina ukweli wowote na serikali inawahakikishia Watanzania kuwepo kwa usalama wa chakula.

Pia, imesisitiza kuwa jukumu la kutoa taarifa za kuwepo kwa njaa ama kutokuwepo kwa njaa ni la serikali, ambayo ina vyanzo vyake rasmi, ambavyo vina jukumu la kufuatilia jambo hilo na kuwasilisha taarifa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, baada ya kuzindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Alisisitiza kuwa hali ya upatikanaji chakula nchini ni tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Kauli hiyo ya serikali imekuja kufuatia kuwepo kwa taarifa zinazotolewa na watu mbalimbali na kuandikwa katika baadhi ya magazeti, kuhusiana na kuwepo kwa baa la njaa nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema mwaka jana, nchi ilikuwa na akiba ya chakula cha zaidi ya tani milioni tatu, ambapo baadhi ya wabunge na wafanyabiashara, waliomba kibali cha serikali ili waweze kuuza nje ya nchi. Alisema serikali ilitoa kibali hicho baada ya kujiridhisha kuwepo kwa akiba ya kutosha.

Majaliwa alifafanua kuwa baada ya kutoa kibali hicho, tani milioni 1.5, ziliuzwa nje ya nchi na serikali ilisitisha uendelezaji wa kuuzwa kwa chakula hicho baada ya kufika tani hizo.

Alisema tani milioni 1.5, zilizobaki zilihifadhiwa kama akiba, ambapo hivi sasa wameruhusu kiuzwe hapa nchini ili kupunguza gharama ya bei sokoni.

“Jambo la njaa na hali ya chakula nchini, nawatoa mashaka Watanzania kwamba, kelele zinazopigwa na watu mbalimbali pamoja na kwenye magazeti, taarifa hizo si za kweli,”alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Alibainisha kuwa chakula kipo cha kutosha licha ya kuwa hali ya mvua inasuasua, lakini hivi sasa mvua zimeanza kunyesha katika maeneo tofauti nchini.

Waziri Mkuu aliwasihi Watanzania kutumia mvua hizo kulima mazao mengi, ambayo ni ya muda mfupi ili kuweza kuwa na chakula cha kutosha katika msimu ujao.

Alisema chakula kilichopo hivi sasa kinategemewa kama akiba katika msimu huu kabla ya kufika msimu ujao.

Majaliwa alisema endapo msimu ujao kutakuwa na uhaba, serikali itatoa utaratibu wa namna ya upatikanaji wa chakula utakavyokuwa.

Kuhusu masoko ya mazao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema baadhi yamepanda bei kutokana na kuwepo kwa uhaba wa chakula katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Uganda, Kenya na Rwanda.

Pia, alisema Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, itatoa taarifa kuhusiana na hali halisi ya chakula nchini na pia kuhusiana na hali ya mvua ili Watanzania waweze kupata ukweli wa hali ilivyo.

Aliwaasa wananchi kupuuza na kutosikiliza kampeni zinazofanywa na wafanyabiasha za kusambaza taarifa za kuwepo kwa njaa nchini.

WAZIRI TIZEBA AZUNGUMZA

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba amesema hali ya chakula nchini inaridhisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk. Tizeba, alisema Tanzania ina akiba ya chakula tani milioni tatu, sawa na asilimia 123.

"Upatikanaji wa chakula miaka yote huwa unatofautiana kutoka eneo moja kwenda lingine. Yapo maeneo yalikuwa na uhaba wa chakula, kuna halmashauri 43, ndiyo zimevuna kiwango cha chini, lakini zingine zilizobaki zimevuma chakula cha kutosha," alisema.

Hata hivyo, alikiri kupanda kwa bei ya chakulam hasa mahindi kuliko miaka mingine yote. "Ni kweli kwa sasa mahindi yamepanda na ndiyo maana hata unga nao upo juu," alisema.

Aidha, alisema kuna baadhi ya wakulima wanaficha mahindi ndani ili wasubiri yapande bei, waweze kuyauza kwa bei ya juu.

Tizeba alitoa tahadhari kwa wananchi na wakulima kwa ujumla, kulima mazao yanayostahimili ukame kutokana na mvua kuchelewa kunyesha.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Tizeba aliwataka viongozi wa siasa nchini kutotumia ukame uliopo kupeleka ujumbe usio sahihi kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment