Monday 16 January 2017

CCM ZANZIBAR KUWATUMBUA VIONGOZI WANAOKIUKA MAADILI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimewaonya baadhi ya viongozi na wanachama wanaowashutumu na kuwadhalilisha viongozi wenzao katika vyombo vya habari na hadharani kinyume na utaratibu wa taasisi hiyo.

Onyo hilo lilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, wakati akitoa mada ya mwelekeo wa uchaguzi mkuu wa CCM mwaka 2017/2022, katika mafunzo maalumu ya siku moja ya viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini B, Unguja, kichama.

Alisema viongozi na wanachama wenye tabia hiyo ndani ya CCM, hawawezi kuvumiliwa na watachukuliwa hatua za kinidhamu kupitia vikao vya maadili vya Chama, endapo atathibitika kukutwa na hatia ya kuwajibika.

Alifafanua kwamba, Chama kikiwa ndio kinara wa demokrasia katika mfumo wa vyama vingi Tanzania, utamaduni wa kukosoana, kuelekezana , kuwajibishana na kufanya maamuzi mazito kwa baadhi ya mambo yasiyokwenda sawa kimaadili na kiuongozi upo, lakini kwa kufuata utaratibu wa vikao rasmi vya kikanuni ndani ya Chama.

“Kuna tabia imezuka kwa baadhi ya viongozi na wanachama ndani ya CCM Zanzibar, wamekuwa wababe kiasi cha kuwatolea wenzao shutuma nzito, tena hadharani na kupitia vyombo vya habari, wakati kuna fursa pana ya vikao vya Chama, ambavyo ndio sehemu pekee ya kuelekezana kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo," alisema.

Vuai aliongeza: "Tabia hiyo hatuwezi kuivumilia, hivyo lazima tukate mizizi mapema kabla haijakomaa na kukiangamiza Chama chetu na wote wanaohusika na tuhuma hizo, kwa sasa tunawachunguza na kuwafuatilia kwa kina ili kujiridhisha na yeyote atakayekutwa na hatia, vikao vya maadili vya Chama vitachukua hatua stahiki bila ya kumuonea mtu.”

Alisisitiza kauli yake na kuahidi kuwa, CCM Zanzibar hakitomvumilia kiongozi yeyote anayevunja maadili ya uongozi kwa makusudi, badala yake kitamshughulikia  bila kujali cheo na umaarufu wake kisiasa.

Aliziagiza kamati za maadili kwa ngazi mbalimbali katika maeneo yaliyozuka migogoro hiyo, kuanza mara moja kutekeleza wajibu wao wa kuwaita viongozi hao  katika vikao vya kikanuni ili kusuluhisha na ikishindikana, wafuate utaratibu na kuwapeleka katika ngazi zingine za maamuzi. 

Alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa Chama na jumuia zake pamoja na wanachama kwa ujumla, kusoma Ibara ya 18 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977, toleo la mwaka 2012, inayoelekeza kuwa ni mwiko kwa kiongozi; "Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa upendeleo, au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa na madaraka hayo.”

Naibu Katibu Mkuu akizungumzia mwelekeo wa CCM, aliwataka  viongozi, watendaji na wanachama kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko ya muundo mpya wa Chama na jumuia zake.

Alisema mabadiliko hayo yanatokana na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kilichokaa Desemba 13, mwaka jana na kufikia uamuzi wa kupitisha mapendekezo ya Kamati Kuu ya kufanya mabadiliko ya muundo wa Chama.

Vuai alieleza kuwa  lengo la kufanyika kwa mabadiliko ya muundo wa Chama ni kuimarisha uhai wa taasisi hiyo kiutendaji na kiuongozi ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi, kulingana na wakati uliopo katika ushindani wa kisiasa.

Baadhi ya mapendekezo yaliyofikiwa katika kikao hicho ni kupunguza idadi ya wajumbe na vikao.

Ilipendekezwa kupunguza wajumbe wa NEC kutoka 388, hadi kufikia 158. Kwa upande wa ngazi ya Kamati Kuu, ilipendekezwa kuwa na wajumbe 24 badala 34.

Vuai alisema mapendekezo hayo yatasababisha kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya Chama na kanuni za jumuia na Chama na kuongeza kuwa, vyeo ambavyo havitakuwemo kikatiba havitaruhusiwa.

Pia, aliwataka  viongozi wanaohusika na vikao vya kuchuja waombaji wa nafasi za uongozi, kufuata maadili ya kikanuni kwa kuhakikisha muombaji ametimiza masharti ya uanachama.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha viongozi na watendaji 487, wa Chama na jumuia wa ngazi za matawi, wadi na majimbo ya wilaya ya Kaskazini “B” kichama.

No comments:

Post a Comment