Monday 16 January 2017

PROFESA MBARAWA AWAONYA WANAOANZISHA VITUO VYA KUHIFADHI KUMBUKUMBU


SERIKALI imezitaka taasisi zake kuachana na mpango wa kujenga vituo binafsi vya kuhifadhia kumbukumbu, badala yake kutumia Kituo cha Serikali cha Kuhifadhia  Kumbukumbu (Data), chenye uwezo na hadhi ya kimataifa.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, baada ya kufanya ziara ya kutembelea kituo cha kimataifa cha kuhifadhia kumbukumbu za kimtandao na makao makuu ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Profesa Mbarawa alisema serikali imetumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya kituo hicho mahiri katika eneo lote la Afika Mashariki na kusisitiza kuwa, taasisi za serikali ni lazima zitumie kituo hicho na kwa zile zenye mpango wa kujenga vituo binafsi, ziachane na mpango huo ambao ni matumizi mabaya ya fedha za umma.

"Natoa agizo kwa taasisi zote za umma, ziachane kabisa na mpango wa kujenga vituo vyao binafsi. Serikali imebeba jukumu hilo, imejenga kituo cha hadhi ya juu kabisa, sote tukitumie kituo hiki.

"Kila taasisi ijikite katika majukumu yake ya msingi, hili la 'Data Center' watuachie serikali kwa kuwa tumeshalitekeleza, hatuwezi kuendelea kutumia fedha nyingine kwa eneo hili," aliagiza Profesa Mbarawa.

Akiwa makao makuu ya TTCL, Profesa Mbarawa aliiagiza menejimenti ya kampuni hiyo kuongeza kasi ya utendaji kazi na ubunifu ili kukabiliana na ushindani uliopo katika sekta hiyo, sambamba na kukidhi kiu ya wananchi ya kupata huduma za shirika lao.

"TTCL mna deni kubwa kwa wananchi. Tumeondoa vikwazo vingi vilivyokuwa vikiwakwamisha na sasa tunataka kuona kasi ya uhakika ya utendaji kazi.

"Tumewalipa Bharti Airtel na kuvunja ubia nao, tumewafutia madeni, tumewakabidhi mkongo wa Taifa wa mawasiliano na Kituo cha Kimataifa cha Kuhifadhia Kumbukumbu mviendeshe. Yote haya yamefanyika kwa nia moja ya kuwajengea uwezo ili mtimize majukumu yenu vizuri," alisema Waziri Profesa Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alipongeza jitihada zinazofanywa na TTCL katika kuboresha huduma zake nchini na kueleza kuridhika kwake na kasi kubwa ya kusambaza huduma za mtandao wa 4G LTE.

Awali, katika taarifa yake kwa Profesa Mbarawa, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, alisema hadi kufikia Januari 16, mwaka huu, mikoa saba ya Tanzania Bara, inapata huduma kwa teknolojia ya 4G LTE, ambayo ni  Dar es Salaam, Dodoma, Pwani, Morogoro, Mwanza, Mbeya na Arusha.

Alisema siku moja kabla ya maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, TTCL ilizindua huduma za 4G LTE mjini Unguja.

Kindamba aliongeza kuwa, kutokana uhusiano wa shughuli za kiuchumi na kijamii baina ya Unguja na Pemba, TTCL inakusudia kupeleka huduma za 4G LTE Pemba katika muda mfupi ujao.

No comments:

Post a Comment