Sunday, 8 January 2017

MWINGINE AUAWA KWA KUFUKUA KABURI LA ALBINO


SAKATA la kufukua kaburi alilozikwa marehemu Sista Osisara, ambaye alikuwa mlemavu wa ngozi, aliyefariki miaka sita iliyopita, limechukua sura mpya baada ya mtu mmoja kuuawa na wananchi wakati akijaribu kulifukua tena.

Usiku wa kuamkia Aprili 4, mwaka huu, mkazi wa Chapakazi, Jonas John(28), alitiwa mbaroni na polisi, ambapo wenzake wawili aliokuwa nao walifanikiwa kukimbia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema tukio hilo lilitokea Aprili 4, mwaka huu, saa 12:00 asubuhi na kumtaja marehemu huyo kuwa ni Yela Amon (30).

Kidavashari alisema marehemu Amon, aliuawa baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa mawe na fimbo, wakati akifukua kaburi hilo la marehemu Sista, aliyefariki dunia Februali 28, mwaka 2010 na kuzikwa Februali 29, mwaka huo.

“Awali, marehemu Amon akiwa na wenzake wawili, walifika walifika makaburini hapo usiku wa Januari 4, mwaka huu, saa 6:30 usiku na kuanza kufukua kaburi la marehemu Sista,” alisema Kidavashari.

Alisema kabla ya kumaliza kazi hiyo, ndugu wa marehemu walishtuka na kupiga kelele za kuomba msaada, ambapo John aliyekuwa ndani ya kaburi, alikamatwa na wananchi hao na kupewa kipigo kikali na sasa anashikiliwa na polisi.

Kwa mujibu wa Kidavashari, kutokana na hali hiyo, wananchi wa eneo hilo waliendelea kulinda kaburi hilo kwa siri na ndipo marehemu Amon aliporudi tena kaburini hapo na kutaka kuendelea kulifukua ili amalizie kazi ya kuchukua viungo vya mwili wa marehemu huyo.

“Ndipo wananchi waliokuwa wamejificha walipojitokeza, kumzingira na kuanza kumshambulia hadi kufariki dunia,” alisema Kidavashari.

Kamanda huyo alisema chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina kwani marehemu na wenzake hao wawili, walikuwa wanataka kuchukua mifupa ya marehemu Sista, ambaye alikuwa mlemavu wa ngozi.

Mwili wa marehemu Amon umehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi, wakati upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo ukiendelea kufanyika.

Katika hatua nyingine, mwanamke mkazi wa Mikumi wilayani Kyela, Hilda Sigara (30), ameuawa na mume wake Rebson Tweve (30-35), kwa kupigwa na nyundo kichwani.

Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea Januari 5, mwaka huu, saa 12:00 asubuhi na chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi.

Inasaidikiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.

Mtuhumiwa Tweve alitoroka baada ya tukio na juhudi za kumsaka bado zinaendelea kufanywa na polisi.
 

No comments:

Post a Comment