Sunday 8 January 2017

WAFUGAJI 50 WANYWA MKONO NA DAMU KUJINUSURU



MTU aliyetambuliwa kwa jina moja la Mzigua, amewatapeli wafugaji takriban 50, kiasi cha sh. milioni tano, kisha kuwatelekeza kwa siku tano katikati ya Pori la Akiba la Selous, Kanda ya Kaskazini Mashariki, eneo la Kingupira.

Wafugaji hao walitoa fedha hizo kwa makubaliano ya  kufikishwa wakiwa na mifugo yao takribani 1,900, katika eneo la Ilonga mkoani Morogoro,  wakitokea vijiji vya Ndundunyekanza, Kipungila na Chumbi, vilivyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa mmoja wa wafugaji hao, Risasi Cherehani, walitoa sh. milioni tano kwa makubaliano kuwa, Mzigua angewapitisha  njia fupi wakiambatana na mifugo yao, ambayo ni ng'ombe 1780, kondoo 200 na punda sita.

"Aliturubuni kuwa atatuonyesha njia za mkato kwa shilingi milioni tano na wala hatukujua kama atatupitisha ndani ya pori hili,"alisema.

Baada ya kutelekezwa, wafugaji hao, ambao walikuwa katika hali mbaya, waliomba msaada kwa ndugu zao, ambao waliwasiliana na uongozi wa Pori la Akiba la Selous, ambao kwa haraka ulifanya jitihada za kuokoa maisha yao.

Kikosi cha askari wa wanyamapori walio chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kiliwapa huduma ya kwanza, maji, uji pamoja na kuwakimbiza hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Baada ya tukio hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, aliwatembelea wafugaji hao kwa ajili ya  kuwapa pole na kuwapelekea chakula, yakiwemo maji na unga.

Aidha, Milanzi  aliagiza wafugaji hao waachiliwe huru huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kupita maeneo ya hifadhi kwa vile ni kosa kisheria na wale wote watakaobainika, watachukuliwa hatua za kisheria.

Pia, Katibu Mkuu huyo aliagiza mtu aliyewarubuni wafugaji kwa kuwapitisha ndani ya hifadhi na kutokomea, lazima asakwe kwa udi na uvumba.

"Sisi kama serikali, kitu cha kwanza ni ubinadamu. Tumewahudumia na sasa natoa tamko la kuwaachia wafugaji wote waliopotea ndani ya pori hili kwa vile mateso waliyoyapata na mali waliyopoteza ni kubwa baada ya kudanganywa na kupitishwa ndani ya Pori la Selous,"alisema.

Akielezea uhalisia wa mkasa huo,  mfugaji mwingine aliyekuwa akiwasiliana kwa njia ya simu na ndugu zao nje ya msafara huo, alisema walianza safari hiyo Jumatano iliyopita.

Mfugaji huyo alisema walikuwa wakitembea usiku na mchana  kwa muda wa siku tano bila kujua wanapitishwa ndani ya hifadhi hiyo, ndipo wakaanza kushikwa na kiu kwa vile maji waliyokuwa nayo yalikwisha.

"Tuliishiwa maji na kila tulipokuwa tukijaribu kumuuliza (Mzigua), alituambia baada muda mfupi tutakutana na maji, lakini tuliendelea na safari bila mafanikio.

"Baada ya mwendo mrefu, ndipo tulipoanza kuanguka na baadhi ya wafugaji walianza kunywa mikojo yao pamoja na damu za kondoo kwa ajili ya kuokoa maisha,"alisema.

Aliongeza kuwa, bila msaada wa kibinadamu kutoka kwa askari wa wanyamapori, wangekufa wote.

"Nawashukuru askari wanyamapori kwa kutuhudumia, bila wao leo hii msingemkuta mtu yeyote hapa, tungekuwa tayari tumeshakufa,"alisema.

Awali,  Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kingupira, Paschal Mrina, alisema walipata taarifa za wafugaji hao kutoka kwa wasamaria wema na uongozi wa wilaya ya Rufiji kuwa, kuna wafugaji  wamepotea ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema baada ya taarifa hiyo, walianza kuwasiliana nao kupitia kwa mfugaji mmoja aliyekuwa na simu na kuunda kikosi maalumu cha doria kwa ajili ya kuwaokoa.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa kanda, walifanikiwa kuwaokoa wafugaji wote na  ilionekana mizoga saba na wengine, ambao hawakuonekana taratibu za kuanza kutafuta zimeandaliwa.

Katibu wa Chama cha Wafugaji mkoani Morogoro, Magembe Makoye, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuacha kuwafukuza wafugaji katika maeneo waliyopo, badala yake  wawatafutie maeneo mbadala ili kudhibiti matukio kama hayo, ambayo yamesababisha hasara na mateso makubwa kwa wafugaji.

Pori la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 na limegawanywa katika kanda nane huku Kanda ya Mashariki  Kipungira ikiwa moja kati  ya kanda kubwa, yenye kilomita za mraba 7,650.
Shughuli zinazofanyika katika pori hilo ni utalii wa picha na uwindaji.

No comments:

Post a Comment