Thursday 5 January 2017

LEMA AZIDI KUGONGA MWAMBA



JITIHADA za mawakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema za kumtafutia dhamana,  zimeendelea kugonga mwamba baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha notisi ya kupinga rufani yao katika Mahakama ya Rufani.

Kufuatia notisi hiyo, iliyosajiliwa Desemba 30, mwaka jana, katika Masjala ya Mahakama ya Rufani Arusha, shauri la dhamana ya Lema sasa litatinga Mahakama ya Rufani katika siku itakayopangwa.

Jaji Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, alitarajiwa kusoma uamuzi wa maombi ya rufani ya upande wa utetezi iliyowasilishwa mahakamani hapo Desemba 21, mwaka jana.

Desemba 28, mwaka jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mbele ya Jaji Salma, iliutaka upande wa Jamhuri kuwasilisha hoja zao Desemba 29,  za  kupinga dhamana ili upande wa utetezi uweze kujibu hoja hizo Desemba 30 na Januari 2, mwaka huu, ilipangwa kuwa siku ya kutoa hoja za ziada kwa pande zote mbili, lakini upande wa Jamhuri haukutekeleza maagizo hayo.

Wakili wa Serikali, Innocent Njau, aliileza mahakama hiyo jana, kuwa upande wa Jamhuri umeshawasilisha notisi ya rufani yao katika Masijala ya Mahakama ya Rufani, hivyo Jamhuri haiwezi kuendelea na shauri hilo Mahakama Kuu.

Baada ya maelezo hayo, Jaji Salma alisema hawezi kuendelea na shauri hilo kwa kuwa limeshawasilishwa mahakama ya rufaa.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Wakili wa utetezi, John  Mallya kwa niaba ya jopo la mawakili wenzake, Petera Kitabala, Sheck Mfinanga, Adamu Janir na Faraji Mangula, alisema mawakili wa serikali wamefanya ‘uhuni wa kisheria’ wa kupinga ombi la rufani yao lisisikilizwe katika Mahakama ya Rufani.

Alisema utaratibu uliotumika haupo kisheria na wamejipanga kuipinga notisi hiyo Mahakama ya Rufani.

“Mahakama ya Rufani ndiyo ya mwisho, hawawezi (mawakili wa serikali) kuendelea kukwepa tena. Tutakutana huko,” alisema.

Wakili wa Serikali, Njau, hakutaka kuzungumza na wanahabari wala kuwasikiliza alipoombwa kutoa ufafanuzi zaidi.

Lema, ambaye ameshakaa mahabusu kwa zaidi ya miezi miwili, tangu alipokamatwa na polisi mjini Dodoma, Novemba 2, mwaka jana, akituhumiwa kwa mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli, alirejeshwa mahabusu katika Gereza la Kisongo, lililoko nje kidogo ya Jiji la Arusha

No comments:

Post a Comment