Thursday, 5 January 2017

DK. SHEIN AWAKOROMEA WAFANYAKAZI WA BANDARI

RAIS Dk. Mohammed Shein ameagiza watendaji waliopewa dhamana ya kuendeleza bandari, kuacha kufanya kazi kwa mazoe.

Dk. Shein alisema hayo jana, katika hafla ya uzinduzi wa vifaa vipya vya kuhudumia mizigo bandarini, iliyofanyika katika Bandari ya Malindi mjini Unguja, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema kwa kuwa bandari ni lango la biashara, lazima wafanyakazi wa Shirika la Bandari waendelee kubuni njia bora za kuongeza ubora wa huduma kwa wale wanaowahudumia na kujitangaza zaidi ili kukabiliana na ushindani uliopo.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa, miongoni mwa masuala ya kuyazingatia ni kuwa waaminifu na waadilifu zaidi, kuepuka urasimu katika kutoa huduma, kujiepusha na vitendo vya rushwa na zaidi kuhakikisha kuwa wateja wanahudumiwa kwa muda mchache bila ya kukiuka taratibu zilizopo.

Aidha, alisema hatua ya ununuzi wa vifaa hivyo ni mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020, ambayo imeanza kutekelezwa kwa kasi kubwa katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuziimarisha bandari za hapa nchini.

“Katika kifungu cha 90 (a) cha Ilani, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya saba, katika kipindi hiki cha pili, tumetakiwa kuiendeleza Bandari ya Malindi kwa kuipatia vifaa vya kuwahudumia abiria pamoja na kukamilisha ujenzi wa bandari mpya ya kuhudumia mizigo katika eneo la Mpigaduri,” alisema Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa katika kipindi hiki cha pili cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba, serikali itaiimarisha na kuiendeleza Bandari ya Mkoani, kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya kuhudumia abiria na mizigo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa serikali inaendelea na mazungumzo na wawekezaji katika utekelezaji wa azma ya kuimarisha gati ya Wete, kwa kuzingatia umuhimu wa gati hiyo kwa serikali, wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba na watumiaji wote wa Bandari ya Wete.

Kwa upande wa mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Shein alisema kuwa serikali itaendelea kuimarisha gati ya Mkokotoni, kwa kukamilisha ujenzi wa geti kwa ajili ya huduma za usafiri wa wananchi, hasa wa Tumbatu na usafiri wa mizigo kwa kutumia majahazi.

Dk. Shein alieleza kuwa, jitihada hizo za serikali kwa jumla zina lengo la kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa katika bandari za hapa nchini.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza juu ya suala zima la usalama bandarini kuwa ni muhimu huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kudhibiti bandari bubu, kwani kuna taarifa kuwa Zanzibar ina bandari bubu zaidi ya 200, katika sehemu mbali mbali.

No comments:

Post a Comment