Thursday, 5 January 2017

CCM YAIBOMOA CHADEMA MAJOHE

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimebomoa ngome ya CHADEMA, baada ya Mwenyekiti na Katibu wake wa kata ya Majohe, iliyoko Pugu, wilayani Ilala, Dar es Salaam, kuhamia CCM.

Hayo yalijitokeza jana, kwenye kata ya Majohe, ambapo wanachama  hao, ambao ni tegemezi kwa CHADEMA, walipohamia CCM na kurudisha mhuri na mpango kazi wa chama hicho wa mwaka mzima.

Wanachama waliohamia CCM ni Andrew Kaseka (Katibu wa Kata ya Majohe), Raphael Revocatus (Mwenyekiti), Nondo Almas, Aziza Ally, Mbogo Kapama na Vaileth Ikangaa. Wengine ni Hamisi Bisumwa (Katibu wa matawi mawili ya Rada na Kichangani ya CUF).

Wakizungumza baada ya kukabidhiwa kadi za CCM, Kaseka alisema: "Mimi ndiye mtendaji mkuu wa CHADEMA kata ya Majohe na nimeamua kutoka kwa sababu hakuna kipya, kumejaa vurugu tupu."

Alisema sera, ambazo alikuwa anazitaka CHADEMA, kwa sasa zipo CCM na zinatekelezwa na Rais Dk. John Magufuli, hivyo haoni haja ya kuendelea kuwepo CHADEMA.

"Nimeamua kurudi nyumbani, baada ya kupata kile nilichokuwa nakitaka. Kile sio chama ni kikundi cha watu wachache ambao ni wapuuzi tu," alisema.

Alisema kwa kuwa amehamia CCM, atahakikisha kata ya Majohe, ambayo ipo CHADEMA inarudi CCM.

Kwa upande wake, Revocatus alisema: "Kazi imeanza na sitawaangusha, nitakuwa bega kwa bega na makada wa CCM, kuhakikisha ushindi wa kata, serikali za mitaa na jimbo vinarudi CCM."

Akizungumza baada ya kukabidhi kadi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Assaa Simba, alisema kuhamia kwa wanachama hao ndani ya Chama, inaonyesha dhahiri kuwa walikuwa hawaichukii CCM.

Alisema UKAWA wataendelea kusambaratika kwa sababu walikuwa hawawaambii wananchi ukweli, badala yake walikuwa wakiwadanganya.

"Nashangaa wanachama wa vyama vya upinzani, ambao bado wapo huko, wanasubiri nini? Rudini nyumbani, milango ipo wazi. Milango yetu haifungwi, ipo wazi muda wote," alisema.

Aidha, aliwaomba wanachama wa CCM kutowaogopa wale wanaohamia ndani ya Chama, bali wawakaribishe na wafanye nao kazi kwa manufaa ya Chama.

No comments:

Post a Comment