Friday 9 September 2016

SPIKA NDUGAI AKERWA NA TIMUA TIMUA YA WABUNGE WA UPINZANI



SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameeleza kukerwa na baadhi ya vyama vya upinzani kufukuza wabunge wake kienyeji na kuvitaka kujifunza kutoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho licha ya kuwa ba wabunge ambao amewaita ‘vichwa ngumu’, haiwafukuzi.

Ndugai alibainisha hayo jana asubuhi bungeni huku akiomba radhi kabla ya kuzungumza kile alichoeleza kuwa kimekuwa kikimkera na kumsumbua sana.

“Naomba kwanza radhi kwa hiki nitakachozungumza maana kinaweza kuwaudhi wengine, lakini naomba nitoe tu ushauri kwa vyama vya upinzani… sipendi kusikia na kuona hii tabia ya baadhi ya vyama vya upinzani kufukuza wabunge kienyeji,” amesema Ndugai.

Ndugai amesema wapinzani wajifunze kwa CCM, kwani hajasikia wakifukuza wabunge, ingawa wapo wabunge wa CCM wengine ni ‘ vichwa ngumu.’

“Ndugu zangu kupata mbunge wa kuchaguliwa si shughuli ndogo. Hawa wabunge wanachaguliwa na wananchi walio wengi tena wengine sio wa vyama husika, halafu wanakaa watu wachache wanamtimua mbunge…jamani kupata mbunge wa kuchaguliwa ni shughuli pevu,” amesema.

Spika Ndugai amewataka wavumiliane na kumalizana tofauti zao ndani ya vyama, badala ya kufukuzana hovyo au kienyeji.

Baada ya Spika Ndugai kumaliza kutoa ushauri wake huo, baadhi ya wabunge walisimama kutaka mwongozo. Hata hivyo, aliwazuia na kuwaeleza kuwa ndio maana aliomba radhi kabla ya kuzungumza kwa kile alichoeleza kuwa yeye ni mlezi wa wabunge wote na hivyo ana haki ya kuwatetea hata wabunge wa upinzani, wanaofukuzwa bila sababu.

Hivi karibuni, Chama cha Wananchi (CUF) kimewasimamisha uanachama baadhi ya viongozi wake akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara, Magdalena Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kaliua.

Hata hivyo, akichangia katika maswali na majibu juzi, Sakaya alisema anaendelea na shughuli zake ndani ya chama hicho.

Mbali ya Sakaya, wengine waliosimamishwa uanachama ni Profesa Haruna Lipumba, Abdul Kambaya ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Ashura Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Katika miaka ya karibuni, kumekuwapo na wabunge ambao wamekuwa wakifukuzwa na vyama vyao na kwenda kusaka haki mahakamani.

Baadhi yao ni aliyekuwa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF), David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na Kabwe Zitto (Chadema).

CHANZO CHA HABARI: GAZETI LA HABARI LEO

No comments:

Post a Comment