UBADHIRIFU wa kutisha unaohusisha mabilioni ya fedha, umefichuliwa kwenye Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ukihusisha uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni.
Wanaodaiwa kuhusika na utafunaji wa mabilioni hayo, walitumia mabadiliko mapya ya usajili wa vitambulisho, yaliyoigharimu serikali kupitia manunuzi yasiyo na tija huku wadanganyifu wakitumia mianya iliyopo kujinufaisha wenyewe kinyume na taratibu.
Kutokana na hali hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, aliagiza wale wote waliohusika na ubadhirifu na udanganyifu wa mabilioni ya fedha, wachukulie hatua kali.
“Ukaguzi umejiridhisha kwamba, uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya taifa,” alisema.
Mkaguzi Mkuu alisema mradi huo unajumuisha mikataba ya manunuzi ya vifaa vya kuboresha vitambulisho vya taifa, ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kama vile ipad, programu na vifaa vya kompyuta, upatikanaji wa vibarua, bima za magari na gharama za kusafirisha na kufunga vifaa vya kusajili raia.
Alisema kutokana na hali ya usajili na kutoa vitambulisho hivyo kuwa mpya, ilisababisha maandalizi hafifu kwa uongozi wa NIDA juu ya kuamua jinsi ya mfumo, ambao ungeweza kutumika vizuri kulingana na uwezo wa mamlaka.
“Kama ilivyobainika kutokana na hali ya usajili na utoaji wa vitambulisho vya taifa kuwa mpya, kulitokana na maandalizi duni ya uongozi wa mamlaka katika kuamua namna mifumo ingefanya kazi vizuri.
“Hali hiyo ilisababisha kuwepo kwa mabadiliko makubwa juu ya maelekezo yaliyoigharimu serikali kupitia manunuzi yasiyo na tija na wakati huo huo kwa wadanganyifu kutumia mianya iliyopo kujinufaisha kinyume na taratibu,” alisema.
Aliishauri serikali iwachukulie hatua kali maofisa wa umma walioshindwa kusimamia kuongoza zoezi la kusajili vitambulisho vya taifa kwa raia wa Tanzania.
Aidha, alisema mamlaka za upelelezi zichunguze viashiria vya udanganyifu vilivyotambuliwa kama ilivyoelezwa kwenye ukaguzi na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.
Pia, alishauri mfumo wa udhibiti wa ndani uimarishwe ili kuhakikisha kuwa malipo ya huduma yanafanyika pale tu huduma inapokuwa imetolewa.
Vilevile, alisema hatua za kinidhamu na za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika waliotajwa kufanya marejesho ya matumizi kwa kutumia nyaraka za wazabuni za kughushi.
Aliongeza kuwa, kiasi cha fedha kilicholipwa kwa huduma isiyotolewa kirejeshwe na wahusika waliotajwa.
WATUMISHI HEWA
Profesa Assad alisema: “Katika ukaguzi, nilibaini taasisi 19, zililipa kiasi cha shilingi bilioni 1,400,554,592, kama mishahara kwa watumishi 260, walioacha kazi, waliokufa, waliostaafu na waliofukuzwa.”
Alisema mishahara hiyo ililipwa kwa kipindi kati ya mwezi mmoja hadi 72, kinyume na Kanuni ya 113 ya kanuni za Fedha za Umma za mwaka 2001 (zilizorekebishwa 2004), inayosema maofisa masuuli watunze nyaraka za watumishi ili watumishi wanaolipwa wawe ni wale waliokuwepo na kufanyakazi.
Mkaguzi mkuu alisema hadi kufikia Januari 2017, kiasi cha sh. milioni 158.3 kilikuwa kimesharejeshwa.
“Malipo ya mishahara kwa watumishi, ambao hawapo kwenye utumishi wa umma ni hasara kwa fedha za umma, hivyo juhudi za serikali zinahitajika zaidi kushughulikia dosari hii,” alisema.
Alisema hali hiyo ni tofauti ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita, ambapo kuna ongezeko kutoka taasisi 16 hadi 19 na kutoka sh. milioni 392,6 hadi sh. bilioni 1.4, sawa na asilimia 257.
“Hili ni tatizo la kimfumo kwenye taasisi za serikali. Ninaendelea kushauri kwamba, maofisa masuuli wahakikishe kuwa fedha zilizolipwa zinarejeshwa Wizara ya Fedha na Mipango,” alisema.
Pia, aliwataka wahakikishe wanaimarisha udhibiti katika urekebishaji wa kumbukumbu za watumishi ili kuzuia upotevu wa fedha za umma.
No comments:
Post a Comment