Na John Kiroboto
UPO usemi wa
Kiswahili unaosema kwamba ‘mwonja asali huchonga mzinga’. Maana yake ni kwamba
mtu akishapata tamu hutaka aendelee kuwa nayo zaidi na zaidi. Ndiyo sababu hata
nzi akishatua kwenye kinyesi au kidonda huwa radhi kufia hapo.
Tabia hiyo iko hata
kwa binadamu wenye uchu wa kupata na kuishi maisha mazuri na kutaka aendelee
kuwa hapo hata kwa gharama ya kupoteza maisha ya mwenzake. Tumeshuhudia
matajiri wakipitia njia hizo na kuwa tayari kuangamiza wengine.
Yupo mfanyabiashara
nchini ambaye alipata kuapa kuwa amepata utajiri alionao kwa gharama kubwa na
hivyo hata kuwa tayari hata kwa sekunde kuupoteza na kuporomosha hadhi yake na
atakuwa tayari kuulinda kwa gharama yoyote ile.
Wapo watu ambao
daima hupenda kuishi kwa kubebwa na hata kunyenyekewa kwa kulipwa fadhila hata
kama mchango wao kwa maendeleo ya watu wengine si mkubwa wa kulingana na ngazi
aliyofikia mlengwa aliyesaidiwa.
Katika nchi hii wapo
watu waliotoa michango yao katika ujenzi wa Taifa na kupewa heshima kubwa na
kuwa miongoni mwa watu wanaoheshimika na majina yao kutajwa kwa heshima kila
wanapokuwa.
Haipingwi, kuwa mwanasiasa
mkongwe nchini Kingunge Ngombale-Mwiru, ana historia ndefu katika ujenzi wa
Taifa hili na hasa ndani ya TANU na CCM, kutokana na kuwa mstari wa mbele
kwenye ujenzi wa vyama hivyo kabla na baada ya uhuru.
Amekuwa katika
serikali kwa awamu zote nne akiwa mshauri wa karibu sana wa marais Julius
Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na akifanya hivyo
hata ndani ya CCM na akishiriki kuandaa ilani na hata miongozo ya chama.
Nafasi zote hizo
zilimjenga na kumpa heshima kubwa licha ya upungufu wa kibinadamu ambao kila
mwanadamu anao, na hapana sababu ya kuuelezea hapa kwani kuna safu zingine
ambazo zitahusika na kumchambua mzee huyu ambaye kaamua kuzima nyota yake
mwenyewe.
Baada ya kuanza
kinyang’anyiro cha kutafutwa mrithi wa Rais Kikwete ambaye atakuwa Rais wa
awamu ya tano, Kingunge hakukaa mbali na mchakato, huku akiibuka ndani ya
CCM na kujinasibu kuwa na mgombea wake ambaye anasema alimkubali kuwa ndiye
pekee anayeweza ‘kuikomboa Tanzania’, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya
Richmond, Edward Lowassa.
Alijitokeza siku
Lowassa anatangaza nia yake ya kuwania urais wa Tanzania kupitia CCM
kwenye mkutano uliofanyika Arusha na kupewa nafasi kubwa ya kumzungumza
na kumsifu Lowassa, jambao ambalo lilizusha gumzo kwa maana ya nafasi aliyokuwa
nayo Kingunge na alivyoamua kumkumbatia mwana CCM mmoja.
Hata Lowassa
alipokatwa katika kura ya maoni ya kuchuja wagombea ndani ya CCM ambapo Dk John
Magufuli alibuka kidedea, Kingunge alionesha waziwazi hasira zake na kudai kuwa
kanuni na Katiba ya CCM vilikiukwa hata kumpata Magufuli baada ya mgombea aliye
na mahaba naye kukatwa.
Juzi nyumbani kwake
Mikocheni, Dar es Salaam, katika hali ile ile ya kusononeka kwa kukatwa kipenzi
chake na kuhamia Chadema ambako hivi sasa ni mgombea urais, Kingunge aliibuka
tena na kuisema CCM kabla ya kutanga kuachana nayo na kuudanganya umma kuwa
hatajiunga na chama hicho.
“Sikubaliani na
mambo yaliyotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM kule Dodoma,
kilichotokea ni kuwadhalilisha wagombea wenye haki…wagombea wamezungushwa mikoa
15 kwa gharama zao na kuishia mlangoni mwa Kamati Kuu, CCM inaamini binadamu
wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa utu wake,” alisema
Kingunge.
Kuzungushwa kutafuta
wadhamini ni utaratibu wa chama ambao mzee huyu alikuwa anaufahamu na bila
shaka alishiriki kuuweka, hivi sasa malalamiko yake hayatokani na utaratibu huu
kufuatwa bali ni kipenzi chake kukatwa.
Kama Lowassa
asingekatwa, hoja ya kuzungushwa kuwa udhalilishwaji isingekuwapo, kwa sababu
roho yake ingetulia kwa kuwa anaamini Lowassa angeshinda urais na yeye
kuendelea kuwa mshauri tena wa Rais katika masuala ya kisiasa na kuendelea
kulia kivulini.
Akizungumza na
wanahabari, alisema anaachana na CCM na hatajiunga na chama chochote. Hapana
uhakika kama hayo yalitoka rohoni, kwa sababu ni wale wale ambao leo wanasema
hiki kesho wanabadilika, ni dhahiri kama baadhi ya vyombo vya habari
vilivyoripoti, anamfuata swahiba wake Lowassa, hivyo atajiunga na Chadema.
Alisisitiza kubaki
kuwa mtetezi wa mabadiliko huku kauli yake ikionesha kuwa wazee hawataki
mabadiliko akiwamo yeye. “Vijana wanataka mabadiliko ukiondoa wale wa UVCCM,
akina mama wengi nao wanataka mabadiliko, wafanyakazi, wakulima, wafugaji,
wavuvi wachimbaji wadogo wa madini, wanafunzi wa sekondari, vyuo pamoja na
wasomi,” alisema Kingunge bila hata kutaja wazee kama yeye.
Mzee huyu aliyekaa
ndani ya chama hicho kwa zaidi ya miaka 60 leo anaibuka na kuishambulia CCM
kuwa imeishiwa pumzi, yawezekana kwa yeye kujipima kiumri akijilinganisha na
CCM ataona ni sawa, huku akisahau kuwa kuna vijana wamekuwa wakiingia kadri
wazee wanavyoishiwa pumzi kama yeye.
Ndani ya CCM
wamepita vijana na wazee wengi na wengine kukaa pembeni wakitoa ushauri wa hapa
na pale, huku akina Kingunge wakiendelea kubaki humo kwa sababu za kutaka
kujihami kiuchumi, lakini pia kwa huruma ya viongozi wa kitaifa wasiotaka
kumwona akiadhirika kimaisha.
Lakini pia Kingunge
amekuwa akijisahau na kutaka kujiona au kujilinganisha na Mwalimu Nyerere
akidhani kuwa kauli yake inaweza kuwa na uzito mkubwa wa hata kuibadili na
kuigeuzageuza CCM kwa mujibu wa matakwa yake. CCM waliliona hilo na kuendelea
naye hivyo hivyo kwa kuheshimu umri alionao na mchango wake kwa chama nyuma.
Vijana wa CCM, damu
changa ya CCM asiyoitambua Kingunge ililiona hilo na kumwona mzee huyu
akikengeuka na hivyo kuamua kumvua ukamanda wa vijana Taifa kwa sababu
hakuonekana kama mtu ambaye bado na msimamo ila anayeendeshwa kimaslahi zaidi.
Ieleweke tu kuwa
Kingunge na wenzake wakiwamo akina Frederick Sumaye , Lowassa, Mgana Msindai,
Makongoro Mahanga, James Lembeli, Hamis Mgeja na wengineo kadhaa, ndio
wamepoteza mwelekeo na kuamua kukumbatia nyuki.
Mwanasiasa huyo
mkongwe akaamua kuishambulia CCM eti inakumbatia matajiri na kusahau kuwa huko
aliko swahiba wake ambaye naye ni tajiri, kuna matajiri ambao pia hawawezi
kuelezea vyanzo vya mali walizonazo licha ya hata kuficha taarifa kwenye
Tume ya Maadili ya Viongozi.
Si siri kuwa haya
yanayiofanyika hivi sasa miongoni mkwa baadhi ya viongozi wa siasa, yanatokana
na kutokuwapo kwa Nyerere, kwa sababu angekuwapo hata Lowassa asingethubutu
kutia mguu kwenye kinyang’anyirio na wala akina Kingunge na Moyo wasingefunua
vinywa kuitukana CCM.
Kingunge alichelewa
sana kutoa tamko alililotoa juzi kwa wanahabari, kwani alitakiwa aondoke au
aondolewe pamoja na mwenzake Hassan Nassoro Moyo wa Zanzibar pale tu walipoanza
kujiumauma na kutafuna maneno yao, huku wakiishambulia CCM kutokana na uchumi
wao binafsi kutetereka. Inajulikana tu kuwa Kingunge na wenzake wana tabia ya
fuata nyuki ule asali. Lakini ajue anaweza kufuata nyuki akakosa asali na
kuambulia manundu usoni.
No comments:
Post a Comment