MWENYEKITI wa Taifa
wa CHADEMA, Freeman Mbowe, anataka kuleta machafuko nchini na hotuba zake za
kichochezi na zinazoashiria hali ya kukata tamaa ndizo zinazonifanya kusema hivyo.
Tuirejee hotuba yake
ya hivi karibuni ambayo aliitoa wakati akiwahutubia Waislamu kwenye Baraza la
Idd la Mfungo Tatu jijini Dar es Salaam.
Hotuba yake ilipewa
uzito mkubwa na gazeti moja litolewalo kila siku ambalo lilimnukuu Mbowe kwa
kuandika “Mbowe amuonya Kikwete.”
Mbowe anasema Rais
Kikwete asicheze na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu,
kwani akifanya hivyo ataliingiza Taifa kwenye matatizo makubwa.
Kwanza inabidi
tuhoji mantiki ya Mbowe kwenda kusema masuala ya uchaguzi kwenye hafla ya
kidini, Je, Mbowe alilenga nini kama sio kufanya kampeni kwa kutumia jukwaa la
dini?
Mbowe anasema “ndugu
zangu Waislamu, namuonya Rais Kikwete asicheze na uchaguzi wa mwaka huu.”
Kulikuwa na ulazima gani wa Mbowe kumuonya Kikwete kwa kutumia mimbari ya dini?
Je, Mbowe hangeweza
kuyasema akiwa kwenye mikutano ya kampeni za UKAWA? Ni wazi kwamba aliwalenga
Waislamu kwa kusudi maalumu.
Hii ni safari ya
pili kwa UKAWA kufanya kosa la kuzigeuza nyumba za ibada kuwa jukwaa la kampeni
kwa lengo la kunasa kura za waumini.
Mara ya kwanza ni
pale mgombea urais wa UKAWA, Edward Lowassa alipokuwa Tabora akiwa kanisani
alinukuliwa kuomba Walutheri wamwombee kwa kuwa tangu nchi hii ipate uhuru
imekuwa ikitawaliwa na marais Wakatoliki, Nyerere alikuwa Mkatoliki, Mkapa
Mkatoliki, safari hii ni zamu ya Walutheri.
Wananchi wengi wenye
kuitakia mema Tanzania waliilaani kauli hiyo inayoashiria ubaguzi wa itikadi za
udhehebu wenye lengo la kuvuta kura za huruma kutoka kwa waumini wa dhehebu
moja.
Hivyo kitendo cha
Mbowe kuhubiri siasa kwenye sherehe za Idd ya Mfungo Tatu hakikutokea kwa
bahati mbaya, bali kilikusudiwa, kilipangwa tangu awali na kudhamiriwa
kutekelezwa kwa lengo maalumu la kupata kura za huruma kutoka kwa Waislamu na
papo hapo kumfitinisha Rais Kikwete na Waislamu.
Maana Mbowe
anaposema ndugu zangu Waislamu namuonya Rais Kikwete asicheze na uchaguzi mkuu
wa mwaka huu ni kama anamshitaki Rais Kikwete kwa Waislamu.
Kama kweli Mbowe
hakukusudia kumshitaki Rais Kikwete kwa Waislamu, basi alidhamiria kuwadhihaki
Waislamu kwasababu Kikwete ni Mwislamu, kwahiyo Mbowe ni kama alipeleka ujumbe
kutoka kwa UKAWA yenye mgombea Mlutheri kwenda kwa Waislamu kuonya kwamba
‘angalieni Mwislamu mwenzenu anacheza na uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu’.
Amebadilisha
wakurugenzi wote katika Tume ya Uchaguzi, Tume iliyopo siyo ile ya mwaka
uliopita na amefanya hivyo huku ukiwa umebaki mwezi mmoja tu uchaguzi ufanyike.
Je, utendaji wa Rais
Kikwete kama kiongozi mkuu wa serikali unahusikaje na dini yake hadi mabadiliko
ya kiserikali yajadiliwe kwenye Baraza la Idd?
Mbowe alikuwa na
maana gani kukosoa utendaji wa serikali kwenye hafla ya kidini? Ni ujumbe wa
aina gani ambao kiongozi huyo alikusudia kuwafikishia Waislamu wakati
wanasherehekea Idd?
Mbowe aliendelea
kusema “hivi karibuni watu wa usalama walifika ofisi za tume hiyo na kumbeba
mkurugenzi aliyebaki wakakaa naye kwa siku tatu aliporudi wakamwamrisha
akabidhi ofisi, sasa tume inaongozwa na vyombo vya dola”.
Je, maneno ya aina
hii ndiyo yanayostahili kwenye mkutano wa dini? Kwanini Mbowe hakuitisha
mkutano na wanahabari ili atoe dukuduku lake?
Yawezekana aliogopa
maswali kutoka kwa wanahabari, akaona ayaongelee hayo kwenye Baraza la Idd kwa
kuwa hatahojiwa chochote, waislamu wataishia kuwa wasikilizaji.
Mbowe anaendelea
kumshitaki Kikwete kwa Waislamu akisema Rais Kikwete ajue kuwa usalama wa nchi
hii umo mikononi mwa wananchi hivyo, wakiamua wanaweza kufanya lolote.
Hii ni lugha ya
uchochezi inayotufanya tuamini kwamba Mbowe alidhamiria kuwashirikisha baadhi
ya waislamu wajumuike kwenye uamuzi wao yaani wajumuike kuunga hicho
walichokiamua kwa siri viongozi wa UKAWA.
Yaelekea viongozi wa
UKAWA wamekwishaamua kwamba wasipoingia madarakani mwaka huu lazima vurugu
itokee. Nasi watanzania wenye nia njema tunawaeleza na tunawaonya kwamba
uongozi wa nchi hii umo mikononi mwa wananchi, ni wananchi ndio wanaoamua nani
awe Rais wao.
Kwahiyo, wao UKAWA
hawana haki ya kuamua kwamba iwe isiwe lazima mwaka huu waingie Ikulu,
wanaoamua nani aingie Ikulu ni wananchi na uamuzi wao ni wa mwisho.
Mbowe aliendelea
kusema “Rais Kikwete anapaswa kuwaacha watanzania waamue wenyewe kwa kumchagua
mtu wanayempenda akishinda apewe haki na si kumnyima.”
Hapa kuna swali,
Mbowe anajua wananchi wanampenda nani na kumchukia nani? Ana kipimo gani cha
kujua wananchi wanampenda fulani na kumchukia fulani wakati haijawahi kuitishwa
kura ya maoni nani anachukiwa na nani anapendwa?
Mbowe aliendelea
kuwaambia waislamu akisema “kwa muda mrefu watanzania wamekuwa wakionewa kwa
kukosa haki, wakinyonywa, sasa wamesema basi, muda umefika wa kulikomboa
Taifa la Tanzania kwa njia ya sanduku la kura”.
Mbowe anawakumbusha
waislamu uonezi na mauaji ya Mwembechai ya mwaka 1998 ambapo Sumaye alikuwa
waziri Mkuu. Askari waliingia msikitini na viatu. Je, akina Sumaye na Lowassa
ndio wa kuwakomboa watanzania na uonezi?
Lowasa akiwa Waziri
wa Nchi katika ofisi ya waziri mkuu ndiye aliyesaini makubaliano ya MOU
(Memorandum of Understanding) ambayo baadhi ya waislamu wanayalalamikia, leo Mbowe
anataka kuwahadaa Waislamu kwamba Lowassa atakuwa mkombozi wao.
Mbowe anazungumzia
ukombozi kupitia sanduku la kura kwani ni lini watanzania walipata uongozi nje
ya sanduku la kura?
Tangu 1958 wananchi
wa nchi hii wameshiriki kwenye uchaguzi mkuu uliowawezesha kuwapata viongozi
wao, kwa mara ya mwisho 2010 ambapo wamempata Rais Kikwete kupitia sanduku la
kura.
Kwa hiyo, uchaguzi
wa mwaka huu (2015) una tofauti gani na chaguzi zilizopita? Watanzania
hawachagui kiongozi wa dini, bali wanamchagua Rais ambaye ataunda serikali
itakayotawala katika misingi ya Katiba na Sheria.
Kisiasa Rais
ataongoza serikali inayotekeleza ilani ya uchaguzi na sera zilizonadiwa wakati
wa kampeni na zilizoiwezesha kushinda na kuingia madarakani.
Kwahiyo, kama kweli
Mbowe amedhamiria kuwaletea Waislamu ukombozi, angenadi sera za UKAWA na
kuthibitisha jinsi zitakavyowakomboa Waislamu.
Kwakuwa hakufanya
hivyo akaishia kukosoa utendaji wa serikali naweza kusema Mbowe aliwauzia
Waislamu bidhaa iliyofichwa ndani ya gunia, haijulikani UKAWA ikiingia
madarakani watawafanyia nini Waislamu wa nchi hii?
Turejee kwenye hoja
yake kuhusu uhamisho na mabadiliko ya wakurugenzi wa Tume.Ilivyo Tume ni asasi
ya dola inayojiendesha kwa uhuru.
Lakini tume
haijiundi yenyewe, wala haijiendeshi nje ya misingi na taratibu za utumishi wa
umma yaani (Public Services na Civil Services). Kwahiyo, serikali inayo haki ya
kuwahamisha na kuwabadilisha.
Serikali siyo
mgombea, wala serikali siyo chama kilichoko kwenye ushindani wa kisiasa kwahiyo
inapotokea serikali imemhamisha mkuu wa mkoa kutoka eneo moja la nchi kwenda
eneo jingine ama inapombadilisha kazi ikampa kazi zingine au kumstaafisha hayo
ni mambo ya kawaida kwenye utumishi (Civil service).
Yanaweza kufanywa
wakati wowote pasipo kujali mazingira ya kisiasa kwa sababu serikali haiongozwi
wala kusukumwa na mazingira ya kisiasa.
Kwa ajili hiyo wako
akina Mbowe na timu ya UKAWA waishie kumvaa Magufuli, kama wameishiwa na hoja
za kushindana na mgombea huyo wa CCM wasitafute upenyo kwa kuivaa serikali.
Waiache serikali
iendelee na utendaji wake kwani duniani kote haitokei serikali ikaacha
kufanya kazi zake kwa kuwahofia wanasiasa. Serikali kubadilisha Wakurugenzi ni
masuala ya ndani sawa na wao CHADEMA walivyo na masuala yao ya ndani.
Mnamo mwezi Februari
na Aprili 2015 walimpitisha Dk. Wilbroad Slaa kama mgombea wao wa baadaye
lakini ulipofika mwezi Julai 27 ghafla wakabadilisha na kumweka Lowassa
waliyemuorodhesha kama fisadi namba 9 kwenye orodha yao ya Mwembe Yanga
waliyoiita “List of shame”.
Je, hayo si mabadiliko
yao ya mambo ya ndani? Kwani serikali haina haki ya kufanya mabadiliko kwa
kadri inavyoona? Hofu ya Mbowe ni nini kuhusiana na mabadiliko hayo? Je, yeye
alitaka mambo yaweje au yafanyike vipi ili aweze kukubali na kufurahi?
Inavyoelekea Mbowe
na timu nzima ya UKAWA wana hofu ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu unaotazamiwa
kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, kwahiyo wanatafuta upenyo wa kutokea.
Nasema haya kwa
kuzingatia kauli ya Mbowe aliyoitoa siku za nyuma na kujiapisha kwamba safari
hii kama CHADEMA isipochukua nchi atajiuzulu uenyekiti.
Kwahiyo, inawezekana
Mbowe na timu nzima ya UKAWA wamejiona hawana hoja za kupiku hoja za Magufuli
kwahiyo wanataka kuandaa mazingira yatakayohalalisha kushindwa kwao.
Maana Wakurugenzi
sio ndio wanaomfanya mgombea yeyote ashinde, kwanini Mbowe aguswe na mabadiliko
yao?
Mbowe anadai kwa
muda mrefu watanzania wamenyonywa, je, wamenyonywa na nani? Wamenyonywa na
watawala?
Yeye Mbowe ambavyo
amekuwa mbunge wa Hai kwa miaka kumi na mitano amewanyonya kiasi gani wananchi
wa Hai?
Mbowe amemaliza
hotuba yake kwa kudai kwamba CCM wamekuwa wakiendesha nchi kwa kufanya ufisadi
mkubwa baada ya kulifilisi shirika la umeme na kusababisha nchi kuingia kwenye
mgawo wa umeme.
Ni kweli enzi za
utawala wa Mwalimu Nyerere Tanzania haikuwahi kuonja mgawo wa umeme licha ya
kutokea mazingira magumu kama ya ukame wa 1974.
Tanzania kwa wakati
huo ilikuwa na viwanda vingi vilivyotumia umeme, lakini watanzania hawakuumizwa
na bili kubwa za umeme kwa matumizi ya nyumbani.
Matatizo ya umeme
tumeanza kuyaonja mara baada ya ujio wa Netgroup Solutions iliyoletwa kama dili
ya wakubwa enzi Sumaye akiwa Waziri Mkuu.
Makali ya umeme
tumeyaonja baada ya ujio wa Richmond ambayo haikuwa na sifa za kuzalisha umeme,
lakini bado Lowassa kama Waziri mkuu aliingilia mchakato wa TANESCO wa kutoa
zabuni, hakusikiliza ushauri wa wataalamu wa TANESCO walioiona Richmond
haina sifa sawa na waombaji wengine, ikaamua itangaze upya zabuni ili kuwapata
wenye uwezo.
Lowassa aliitisha
orodha ya wazabuni wote ofisini kwake kama Waziri mkuu na ndipo Richmond
ilipoibuka kidedea wakati wataalamu waliikataa.
Mbowe anakiri ukweli
kwamba baada ya utawala wa Nyerere (1960-1985) watanzania hatukuonja matatizo
ya umeme, bali tumeanza kuwa na umeme wa kuungaunga baada ya ujio wa kampuni
mbili za Netgroup Solution na Richmond ambazo zimeifilisi TANESCO.
Hapa ndipo linaibuka
swali ‘Sumaye kampeni’ meneja wa UKAWA na Netgroup Solution na Lowassa aliye
mgombea wa UKAWA na Richmond, kweli hawa ndio wa kuleta ukombozi nchini?
Kweli hawa ndio wa
kuwakomboa watanzania na kuwaondolea madhara ya kunyonywa na kufukarishwa?
Watawakomboa watanzania kwa mbinu gani na kwa msukumo upi?
Walipokuwa
madarakani kwenye nafasi ya Uwaziri Mkuu walisukumwa kujitajirisha zaidi ndio
maana walibuni miradi hewa kama ya “Speed governor”, Netgroup Solution, na
Richmond. Leo hawawezi kuwashawishi watanzania wenye kumbukumbu zao wawaamini
na kuwakabidhi nchi.
Walipokuwa
madarakani hawakuwasikiliza wananchi, watakapoingia tena hawatamsikiliza yeyote.
Sumaye
hakuwasikiliza wafanyakazi wa TANESCO ambao waliomba kwamba ikiwa TANESCO
inawekwa chini ya menejimeti mpya, basi wao walipwe mafao yao.
Lowassa naye
hakuwasikiliza wataalamu wa TANESCO walioiona kampuni ya Richmond haina sifa ya
kupewa tenda ya kuwapatia watanzania umeme.
Je, hawa kweli ndio
wanastahili kuitwa wakombozi kwasababutu ya kuhubiri mabadiliko? Ni kweli
mabadiliko tunayataka lakini hayataletwa na Lowassa.
0754 425371
No comments:
Post a Comment