WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ameagiza
kuhamishwa kwa Meneja wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kidatu, Manfred Ndyalu
kwa kushindwa kutoa taarifa mapema, baada ya kuchomoka kwa waya na kusababisha
mitambo iliyobaki kuzidiwa.
Pia, amemtaka Meneja Mkuu wa Usimamizi na
Uzalishaji Umeme, Abdallah Ikwassa, kuhakikisha kuwa mashine zote zinafanyakazi, vinginevyo aachie ngazi
kutokana na kutokufanya majukumu yake ipasavyo.
Vilevile, amemuagiza Naibu Mkurugenzi wa
Usafirishaji, Kahitwa Bishaija, kuhakikisha mfumo wa kusambaza umeme wa Ubungo,
unaanza kufanyakazi mara moja, vinginevyo ajitafakari na kuchukua hatua mara
moja.
Kauli hiyo aliitoa jana, alipotembelea mitambo ya
Umeme ya Ubungo na ule wa Kinyerezi 1, baada ya kutokea kwa hitilafu ya umeme,
iliyosababisha kukatika kwa umeme nchi nzima.
Dk. Kalemani alisema, wanamuhamisha meneja wa kituo
hicho, kutokana na uzembe alioufanya wa kushindwa kutoa taarifa mapema ya kuchomoka
kwa waya na kusababisha hitilafu kwenye gridi ya taifa.
"Tumemuelekeza mkuu wake amuondoe kwenye kituo
hicho mara moja ili hali hiyo isijirudie tena na ili tuwe na wafanyakazi
wachache wenye uweledi," alisema.
Kuhusu Naibu Mkurugenzi wa Usafirishaji, alisema
anatakiwa kujitathmini mwenyewe kutokana na kushindwa kusimamia mfumo wa Ubungo, kuhakikisha unafanyakazi.
Pia, alisema Meneja wa Usimamizi na Uzalishaji
Umeme, anatakiwa ajitafakari mwenyewe kutokana na mitambo mingi ya umeme
kutofanyakazi.
"Kutokana na hali hiyo, mitambo mingi ya
kuzalisha umeme na vyanzo vingi vimeshindwa kufanyakazi, lakini nashukuru
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), walitoa taarifa ya kuwaomba radhi
wananchi," alisema.
Hata hivyo, alisema wanaendelea kufuatilia chanzo cha
tatizo hilo ili kuweza kulitatua mara moja.
"Tumefuatilia maeneo yote ambayo tumehisi yana
tatizo, tumeenda kwenye mfumo wenyewe Ubungo ili kuweza kugundua chanzo cha
tatizo, lakini tumekuta mfumo bado unafanyiwa marekebisho ya kuongezewa nguvu,
taratibu zinaendelea.
"Pia, tukaenda Kinyerezi 1, ambako sasa kuna
mashine haifanyikazi, nayo itafanyiwa matengenezo, lakini kubwa ni valvu moja,
ambayo imesababisha mtambo wa Kinyerezi ushindwe kufanyakazi, jitihada
zinaendelea," alisema.
Alisema marekebisho yanaendelea na kwa sasa umeme
unapatikana nchi nzima, baada ya gridi ya taifa kurejea, ambayo imerudi tangu
usiku.
"Lakini hata hivyo, yapo maeneo machache
ambayo hayapati umeme wa kutosha kwa sababu mtambo mmoja wa Ubungo 11, wenye
uwezo wa kuzalisha umeme megawati 129, haujaanza kufanyakazi.
"Nimewaelekeza wataalamu wafanyekazi usiku na
mchana leo (jana), mpaka mtambo wa Ubungo wenye megawati 129, nao uweze
kufanyakazi. Wamenihakikishia kwamba, mpaka leo saa nne asubuhi, mtambo wa Ubungo
11 nao utakuwa unafanya kazi," alisema.
Kutokana na hali hiyo, alisema Wizara na TANESCO
watahakikisha leo, saa 5 asubuhi, maeneo yote yaliyobaki yanapata umeme wa
uhakika.
"Yale matengenezo yaliyokuwa yanaendelea ya
kurekebisha mashine, nazo zitaendelea na utaratibu wake kama kawaida.
Tunawaomba radhi wananchi kwa matatizo yalitokea," alisema.
No comments:
Post a Comment