Monday, 21 September 2015

MAGUFULI APATA MAPOKEZI MAKUBWA CHATO






NA CHARLES MGANGA, CHATO 

MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, jana alipata mapokezi makubwa ambayo yaliufanya uwanja wa mpira wa Chato kutapika.

Dalili za kupata mapokezi hayo zilianza kuonekana tangu siku ya Ijumaa alipowasili wilayani humu.

Siku hiyo, Dk. Magufuli akiwa njiani kwenda Chato akitokea Biharamulo, alisimama mara kadhaa kuwasalimia wananchi na kuwaomba wamchague awe rais wa awamu ya tano.

Alipofika kwake (Chato), Dk Magufuli alipokelewa na wananchi wengi huku wakitaka kumuangalia na angalau kumsogelea kwa karibu.

Katika mkutano wa jana, watu walianza kumiminika kwenye uwanja huo tangu asubuhi licha ya kuambiwa mkutano huo ungefanyika mchana.
Kila kona ya mji wa Chato, ilipambwa kwa rangi za njano na kijani zinazotumiwa na CCM.

Barabarani wananchi walionekana kukimbia kuwahi angalau nafasi za mbele karibu na jukwaa kuu washuhudie yanayojiri.

Hata hivyo, wapo waliOkuwa wakiwasili uwanjani kwa staili ya maandamano huku wakipeperusha picha za Dk. Magufuli na wengine kujipamba kwa kuvaa bendera za CCM.
Kabla ya Dk. Magufuli kuwasili, wasanii mbalimbali walianza kutumbuiza kwa maana ya kuwaweka tayari  wananchi kabla ya mgombea kuhutubia.

Miongoni mwa waliotumbuiza ni Rutta Bushoke, ambaye aliimba nyimbo za kuifagilia CCM na Dk. Magufuli kwamba ndiye anastahili kuwa rais.
Wasanii wengine waliotumbuiza ni bendi ya TOT Plus, walioimba wimbo wa mbele kwa mbele.
 
Saa 7.45, Dk. Magufuli aliwasili katika uwanja huo maarufu kama Mazaina akiwa kwenye gari ya wazi. Mgombea huyo aliongozwa na msafara mrefu ukisindikizwa na lundo la bodaboda.

Wakati huo, TOT plus waliendelea kuwatumbuiza watu waliofurika uwanjani hapo kumpokea Dk. Magufuli, huku wakiimba kwa ishara ya kuonyesha picha, vipeperushi na bendera za CCM.

Baadaye, wasanii wengine walipanda jukwaani akiwemo Chege na Temba, Young D na Wanamchele wa Mwanza.

Wengine ni msanii Shilole, Mr Blue, huku kundi la Ze Komedy likikonga nyoyo za mashabiki. Msanii Masanja aliigiza sauti ya mgombea kwa namna anavyozungumza katika mikutano yake.

Leo, Dk Magufuli, ataanza kampeni mkoani Kagera. Mikoa ambayo  mgombea huyo, ameshafanya kampeni ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Tanga, Mara, Simiyu na Tabora.

No comments:

Post a Comment