KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka wakazi
wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, kutofanya makosa ya kuchagua mbunge na madiwani
kutoka upinzani.
Amesema wagombea wa vyama hivyo hawana sera wala dhamira
njema ya kuwatumikia watanzania na badala yake wachague wagombea wa CCM kuanzia
rais, wabunge na madiwani.
Aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano wa kampeni za
kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Innocent Shirima,
mgombea urais Dk. John Magufuli na madiwani wa chama hicho.
Alisema CCM ndio chama pekee kinachoweza kuwaletea
maendeleo ya haraka, kutatua kero zao mbalimbali na kuongeza kuwa, Serikali ya
Awamu ya Tano chini ya Dk. Magufuli, itafuta sheria kandamizi zinazowaumiza
wananchi.
Sheria hizo ni ile ya kuzuia wananchi wasikate miti
ambayo wameipanda wenyewe ili waweze kujikwamua kiuchumi, akisema ni jukumu la
mbunge na madiwani wa CCM kuhakikisha sheria zote kandamizi zinafutwa.
"Pia kuna sheria ya kifaa cha kuzimia moto kwenye
magari, kimsingi gari nimeinunua mwenyewe, nina bima kwanini nilazimishwe
kununua kifaa hicho...nani kawaambia gari yangu itaungua?” alihoji Kinana.
Alisema kuwa inashangaza sheria ya kuzuia kukata miti
kuwa na urasimu mwingi ukiwemo wa wananchi kutakiwa kuomba kibali kuanzia ngazi
ya kijiji hadi halmashauri na mlolongo mrefu wa kukipata kwake.
Aliwataka wabunge na madiwani ambao watachaguliwa katika
uchaguzi ujao, kuhakikisha wanadhibiti michango holela shuleni ili kuleta
mabadiliko ya kweli kwa Taifa.
"Serikali imefuta ada katika shule za msingi na
sekondari, lakini walimu wamekuwa wakibuni michango mbalimbali kwa maslahi yao
binafsi jambo ambalo limekuwa likiwakandamiza wazazi," alisema.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Nzega Vijijini,
Dk. Hamisi Kigwangala, aliwataka wananchi kuepuka kugawanywa kwa misingi ya
dini na ukabila.
Naye Shirima aliwaomba wananchi wa Vunjo kumpa kura
nyingi awe mbunge wao ili aweze kutatua changamoto zinazowakabili akiahidi
kuhakikisha wananchi wananufaika na mapato yanayotokana na Mlima Kilimanjaro,
kuboresha miundombinu ya elimu, afya na maji.
No comments:
Post a Comment