Tuesday 24 October 2017

JPM: WAPUUZENI WANAOPOTOSHA TAKWIMU ZA SERIKALI




RAIS Dk. John Magufuli, amewataka watanzania kuendelea kuwapuuza wapotoshaji wa takwimu rasmi za serikali, wanaodai mapato ya serikali yanashuka, tofauti na inavyoelezwa na mamlaka husika.

Amesema lengo la watu hao ni kuliondoa taifa kwenye mwelekeo wa kujenga uchumi kwa kuwachonganisha wananchi na serikali yao, inayofanya jitihada kubwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.

Rais alisema vyombo vya ulinzi na usalama, vinapaswa kuwaangalia watu hao na kwamba ana kumbukumbu juu ya uwepo wa sheria ya kudhibiti wapotosha takwimu, ambayo inapaswa kutekelezwa, ikiwezekana wahusika wafikishwe mahakamani kujieleza.

Alitoa kauli hizo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza kwenye hafla ya kuwatunuku vyeti wajumbe wa kamati zilizofanya uchunguzi wa kiwango, aina na thamani ya madini katika makinikia na baadae kufanya mazungumzo na Barrick Gold Mine kwa mafanikio makubwa.

Dk. Magufuli alisema, kuhusu makubaliano ya biashara ya madini, mpaka sasa kazi kubwa, ya hatari imefanywa na watu wenye uzalendo na waliotoa maisha yao kwa ajili ya taifa, hivyo ni jambo la ajabu kwa mtu kusema taifa limeliwa, kwa sababu ya manufaa binafsi.

"Unaweza kuhoji uzalendo wao, watu wamejitoa maisha kwa ajili ya rasilimali za taifa hili, halafu watu fulani wanakuja na kusema eti tunaliwa kwa sababu tu wamepewa kitu chochote kwa ajili ya matumbo yao, hii haikubaliki, nawaomba tutangulize uzalendo," alisema.

Rais Magufuli alifafanua kuwa mtu hawezi kusema serikali inapindisha uhalisia kuhusu takwimu za mapato, wakati kuna miradi na mikataba lukuki imetekelezwa na mingine naendelea kutekelezwa na serikali hiyo hiyo kwenye sekta, maeneo mbalimbali nchini.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo na mikataba kuwa ni ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, Ununuzi wa ndege sita kwa mpigo, ongezeko la fedha kwenye bajeti ya afya, ujenzi wa barabara za lami na usambazaji wa umeme vijijini (REA); na kuhoji kama kweli kusingekuwa na ongezeko la mapato, serikali ingewezaje kuyafanya yote hayo.

"Kwa mfano kwenye mradi wa Stingler Gorge ambao tangu enzi za Hayati Baba wa taifa ulifikiriwa, zimejitokeza kampuni zaidi ya 79 kwa ajili ya kuomba zabuni ya ujenzi, haya yote tunayafanya kwa sababu mapato yapo, kwa hiyo inashangaza watu wakipotosha," alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa mafanikio yaliyopatikana, Watanzania wamethibitisha kuwa ni taifa linalopaswa kutoa misaada na si kuomba misaada hivyo kuna ulazima wa kushirikiana ili manufaa yanayopatikana kwenye sekta ya madini yawe kwa usawa tofauti na ilivyokuwa awali.

Pia, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wajumbe wote wa kamati wakiongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na kuwaita watanzania kweli, wazalendo wenye mapenzi mema na nchi yao licha ya kuweka maisha yao hatarini.

Alisema, kazi waliyoifanya ni kubwa, ya kutisha ambayo bila Mungu wasingeikamilisha na kwamba hata yeye rais, mtikisiko alioupata muda wote wa mazungumzo baina na serikali na kampuni za madini zilizohusika na makinikia, ulikuwa si wa kawaida lakini alikuwa tayari kukabiliana nao kwa kuwa amejitolea maisha yake kwa ajili ya wapigakura wa Tanzania.

"Hii kazi ni kazi mbaya, hawa walijitolea maisha yao kwa sababu hata mimi mtikisiko nilioupata naujua mwenyewe lakini nilijipa moyo kwamba lolote ninalopitia, sijali ili tu matokeo mazuri yawe kwa ajili ya watanzania walionipigia kura niwe rais wao," alifafanua.

Alizitaja faida za makubaliano ya Barrick na Serikali ambayo yametajwa kuwa ya karne kibiashara kwamba pamoja na zingine, ajira kwa watanzania migodini zitaongezeka, kutakuwa na ulipaji wa kodi na ushirikiano kwenye usimamizi wa migodi kwenye ngazi za utawala utakuwa wa ubia.

Rais Magufuli aliongeza kwa kuwashukuru wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kukubali kulifanyia kazi vizuri suala la Hati ya Dharura, iliyohusu kupitisha mapendekezo ya serikali kwenye sheria za madini, ambayo baadhi ya wabunge waliona haina umuhimu lakini matokeo yake ndio yameipa Tanzania heshima kwenye ulinzi wa rasilimali zake.

"Ninawashukuru sana wabunge, mmeonyesha uzalendo mkubwa kwenye kupitisha sheria hii ya madini lakini pia wananchi tunawashukuru kwa uvumilivu wenu, mmesikia mengi lakini bado mmeendelea kuiunga mkono serikali," alisema rais.

Aliahidi kuendelea kutekeleza yale aliyoyaahidi kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi wakati akiomba ridhaa ya wananchi mwaka 2015 na kwamba siku moja wasiomuelewa leo, watakuja kumwelewa nia yake kwa watanzania.

MAZUNGUMZO TANZANITE, ALMASI
Dk. Magufuli alisema, baada ya mazungumzo ya dhahabu, kamati husika, inapaswa kuanza kushughulika na Tanzanite na Almasi ambapo alimtaka Profesa Kabudi na timu yake kuanza mara moja mazungumzo na wahusika.

Alisema anafurahishwa na dalili za mafanikio zilizoanza kujitokeza baada ya kampuni ya Tanzanite One inayohusika na biashara ya Tanzanite, kusema ipo tayari kwa mazungumzo pale itakapohitajiwa kufanya hivyo na serikali.

"Mwenyekiti naomba kazi ianze na tayari Tanzanite One wamesema wapo tayari kwa mazungumzo," alisema Rais Magufuli.

AWAITA WAFANYABIASHARA
Kwa kuonyesha kuwajali wafanyabishara wa ndani, Rais Magufuli alisema, huu ndiyo wakati wa kufanya biashara kwenye sekta zote nchini kuanzia nishati, madini na viwanda.

Alisema serikali yake inawapenda wafanyabiashara na inaamini wana uwezo wa kumiliki hata migodi mbalimbali hivyo milango iko wazi kwa wao kuchangamkia fursa hiyo ya kulijenga taifa lao kupitia sekta ya biashara.

Rais Magufuli, aliutambua uwepo wa Dk. Reginald Mengi na Godfrey Simbeye wa TPSF ambao aliwataka kuufanyia kazi ujumbe wake huku akiwataka wananchi na Kituo cha Uwekezaji (TIC), kuitangaza Tanzania na fursa zake za uwekezaji kokote duniani.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye hafla hiyo, baadhi ya waliyohudhuria  wakiwemo viongozi wa dini, wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wa vyama vya upinzani walisema serikali inastahili pongezi kwenye jitihada ambazo tayari zimefanyika kulinda rasilimali za taifa na ambazo bado zinaendelea kufanywa.

Mussa Azzan Zungu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Almasi alisema, wameridhishwa na kazi iliyofanywa na kwamba, Rais Magufuli ni kiongozi ambaye watanzania wanapaswa kujivunia kwa kumuunga mkono kwenye kila jitihada anayoifanya kulijenga taifa la Tanzania.

Naye Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Ally, alisema viongozi wa dini hawana cha kumlipa rais zaidi ya kumuombea afya njema ili andelee kuwatumikia watanzania kwenye masuala mbalimbali.

Alisema Dk. Magufuli hatakiwi kusikiliza maneno ya mitaani, kwa sababu kwa yeyote anayefanya wema kwenye masuala yenye maslahi, hakosi kulaumiwa na wengi ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa wakinufaika kwayo.

"Wewe rais wetu ni mwema kama ambavyo vitabu vya dini vimesema kuwa taifa linalohitaji matengenezo, linahitaji mtu mwema hivyo sisi tunaamini tutakuwa wema pia kwa sababu yako, usiwasikilize wanaokulaumu... kalaumiwa Mwenyezi Mungu, Mitume na watu wema zaidi," alisema.

Profesa Ibrahim Lipumba kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa, alisema upinzani ulipiga kelele suala la mikataba mibovu ya usiri kwenye sekta ya madini na kwamba ni ajabu kama watu hao hao wataanza kupinga yanayofanywa na serikali kwa sasa.

Alitahadharisha watanzania watakaopata fursa ya kuiwakilisha Tanzania kwenye ubia na kampuni za kigeni za madini kuwa watangulize uzalendo ili kipande cha faida kinachostahili kwa serikali kitolewe kwa weledi na si kwa dhuluma.

"Unaweza kushangaa mgawo wa faida unaambiwa ni asilimia 0, sasa sifuri ikigawanywa 50 kwa 50 unaweza kuona tutapata 0 wakati labda kuna faida kubwa tu ilipatikana ikafichwa kutokana na ukosefu wa weledi wa watu wetu," alisema.

Alisema utanzania kwenye masuala ya maendeleo daima unapaswa kuwa mbele kwanza halafu vyama baadaye hivyo Rais Magufuli anatakiwa kuendelea kushikilia hapo hapo kwa mashali ya taifa.

Waziri wa Madini, Angella Kairuki, kwa nafasi yake alisema, ataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na kamati za madini zilizotunukiwa vyeti jana na rais, ili kudhibiti upungufu uliopo ikiwemo utoroshwaji wa madini ili sekta ya madini iendelee kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa.

"Tunakupongeza sana mheshimiwa rais kwa kazi nzuri ambayo imefanyika, sisi kama wizara mpya tunaahidi kuendelea kupambana na ulinzi wa rasilimali zetu za madini kwa kuziba mianya yote ya utoroshwaji wa madini kwenye maeneo yote," alisema.

Wajumbe waliotunukiwa vyeti na rais jana ni Mwenyekiti Profesa Palamagamba Kabudi, Spika Job Ndugai aliyewakilishwa na mke wake Fatma Ndugai, Profesa Abdulkarim Mruma, James Mgosha, Dk. Yamungu, Geofrey Mwambe, Adolph Ndunguru, Profesa Andrew Luoga, Kasmir Kisaki na Andrew Massawe.

Wengine ni Lusajo Asubisye, Tedy Luasha, Ardegen Mwaipopo, Moses Moses, Royal Lienga, Andrew Mwangakala, Michael Kambi, Profesa Longinus Lutasitara na Dk. Oswald Mashindano.

Pia, Gabriel Malaba, Utano Kisaka, Profesa Rwanura Ikinwa, Profesa Buchweshaiga, Dk. Athuman Ngenya, Dk. Joseph Philip, Dk. Ambrose Matolo, Mohammed Makongoro na Henry Gombera nao walipewa vyeti.

No comments:

Post a Comment