Monday, 2 January 2017

VISIWA VYOTE TANZANIA BARA KUPATIWA UMEME



SERIKALI itavipatia umeme wa gridi ya taifa na nishati jadidifu visiwa vyote vya Tanzania Bara, ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Iseni, Mfunzi, Lugata (kisiwani Kome) na Mwabayanda, wilayani Sengerema, mkoani hapa.

Alisema hakuna taifa duniani linaloweza kuendelea iwapo wananchi wake hawana uememe wa uhakika, ndiyo maana serikali ya awamu ya tano inataka kuharakisha nishati hiyo vijijini ili wananchi wapate maendeleo ya haraka.

“Tanzania tunaelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati, hatuwezi kufikia uchumi wa kati iwapo wananchi hawatakuwa na nishati ya umeme, ndiyo maana serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli inakusudia visiwa vyote vya Tanzania Bara ndani ya miaka mitatu viwe na umeme,”alisema Profesa Muhongo.

Alifafanua kuwa visiwa hivyo ni vilivyopo katika Bahari ya Hindi, Ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria, ambalo lina visiwa vingi, kikiwemo cha Kome, kitakachoendelea kusambaziwa umeme chini ya mpango wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu.

Alisema REA awamu ya pili iliyomalizika mwaka jana, ilifanya vizuri, lakini awamu ya tatu inayotarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwaka huu, itafanya vizuri zaidi kwani mwaka huu wa fedha, serikali imetenga bajeti ya sh. trilioni moja, kwa ajili ya nishati hiyo ili wananchi wajiandae kuitumia kwa ajili ya maendeleo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Miradi wa REA nchini, Emmanuel Yesaya, alisema chini ya mpango wa REA awamu ya tatu, vijiji vyote nchini vitapatiwa umeme wa gridi ya taifa na wa mionzi ya jua kwa vile vilivyoko visiwani, ambavyo haitakuwa rahisi kupeleka umeme wa gridi.

Alisema kwa wilaya ya Sengerema, vijiji 38, vikiwemo Isenyi na Nfunzi,
vitapatiwa umeme wa sh. 27,000, kutoka gridi ya taifa kama ilivyokuwa kwa mradi wa REA awamu ya pili.

Awali, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Amos Maganga, aliwaomba radhi wananchi wa Kome baada ya kulalamika kuwa Desemba, mwaka 2016, ikiwemo siku ya Krismas, umeme ulikuwa ukikatika mara kwa mara.

“Ni kweli umeme ulikuwa ukikatika, naomba mtuwie radhi, sababu kubwa ni kubadilisha njia za umeme zenye msongo wa KV 220 kufikia KV 400, ikiwemo ya Shinyanga na Mwanza, ambayo inahudumia hadi kisiwa hiki.

“Tunajenga njia nyingine ya kutoka Kahama-Geita ili matatizo ya aina hiyo yanayoweza kutokea Geita, yasiwakumbe kwa kuwa sasa mnatumia njia moja kutoka Mwanza,”alisema.

No comments:

Post a Comment