Monday, 2 January 2017
DK. TULIA AWATAKA WATANZANIA KUACHA KUTENDA MAOVU
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Akson, amewaomba Watanzania kuacha kutenda maovu, badala yake wajikite katika kufanyakazi za kujenga nchi ili kwenda pamoja na kauli mbiu ya serikali ya 'Hapa Kazi Tu' kwa lengo la kupata mafanikio katika mwaka mpya wa 2017.
Amesema jamii iliyojikita katika kufanya matendo yasiyompendeza Mungu, itaangamia hivyo ni muhimu kwa wananchi kuacha kutenda vitendo hivyo visivyokuwa na maslahi kwa jamii.
Dk. Tulia aliyasema hayo juzi, kwenye mkesha maalumu wa kuliombea Taifa, uliofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Naibu Spika, ambaye alikuwa akimwakilisha Rais Dk. John Magufuli, alisema ni muhimu kwa Watanzania kuacha matendo mabaya na kujielekeza katika kuliombea taifa.
“Jamii isiyofuata matendo ambayo Mungu ameyaagiza, itaangamia, hivyo katika mwaka huu ni vyema tukafanyakazi kwa kuzingatia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, ili kufikia mafanikio,” alieleza Dk. Tulia huku akinukuu baadhi ya vifungu vya Biblia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkesha huo, Askofu Godfrey Malassy, alisema kwa muda mrefu walikuwa wakimuomba Mungu kupata kiongozi, atakayekuwa akipambana na kuyachukia maovu, hivyo wataendelea kumuombea Rais Dk. Magufuli, kwani ameonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na vitendo hivyo.
“Ni jukumu letu kulinda na kuitetea tunu ya amani kwa kila Mtanzania bila ya kujali itikadi, dini, ukabila na hata utaifa, kwani taifa ambalo halina amani, haliwezi kusogea mbele kimaendeleo ,” alisema Malassy.
Aidha, alisema sadaka itakayotolewa katika mkesha huo, itapelekwa kwenye maeneo ya watu wenye mahitaji maalumu, ambapo kwa mwaka huu, itapelekwa Tabora Vijijini, ambapo wananchi wenye mahitaji ya umeme, watapelekewa vifaa vya umeme wa jua kwa ajili ya nishati hiyo.
Alisema watu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Rwanda na Kenya, watakuja nchini kuungana na Watanzania kupitia mkesha kumshukuru Mungu kwa mambo aliyowatendea, ikiwa ni pamoja na kumuombea Rais Magufuli ili aweze kuendelea kutimiza juhudi zake za kuliongoza taifa.
Mkesha huo mkubwa wa kitaifa wa dua maalumu, hunafanyika kila mwaka katika mikoa zaidi ya 10, ikiwemo Zanzibar na mwaka huu ulikuwa mahususi kwa ajili ya kuliombea Taifa amani na kumuombea Rais Dk.Magufuli ili kuendelea kutimiza majukumu yake.
Viongozi wengine walioombewa ni Makamu wa Rais Samia Suhuhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam, waliohudhuria mkesha huo, walisema wananchi wanapaswa kuungana pamoja kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha taifa kuingia mwaka 2017, kwa amani na utulivu.
Walisema amani na utulivu ni vyema vikadumishwa, hivyo ni muhimu kuwaombea viongozi kwani wao ndio wenye kuhimiza kudumishwa kwa msingi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment