Monday, 2 January 2017

WALIOWEKEWA X KIMAKOSA HAWATABOMOLEWA NYUMBA ZAO

SERIKALI imesema itazifuta na kuziondoa alama za X kwenye nyumba, ambazo ziliwekwa kimakosa kwa ajili ya kubomolewa.

Nyumba hizo ni zile ambazo zilijengwa umbali wa mita 600, kando kando ya mifereji ya maji na kingo za mito, kinyume na sheria ya utunzaji wa mazingira.

Aidha, serikali imeliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuhakikisha linasimamia sheria na taratibu za mazingira.

Hayo yalisemwa jana, Dar es Saalam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira,January Makamba, wakati akikagua ujenzi wa mradi wa mifereji ya maji taka na kuta za kingo za bahari.

Makamba alisema serikali imedhamiria kutetea na kuwathamini Watanzania wanyonge, ambapo inatarajia kutumia mfumo wa ushirikishaji kwa wananchi ili kutatua usumbufu huo wa ubomolewaji wa nyumba.

“Nadhani kila Mtanzania anafahamu kwa kiasi gani serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, inavyotetea wanyonge, hivyo kwa sasa serikali imeamua kufanya mfumo wa ushirikishaji ili kuangalia namna ya kutatua kero hiyo,”alisema.

Aliongeza kuwa licha ya serikali kufanya maamuzi hayo ya kusitisha kubomoa nyumba hizo, ambazo ziliwekwa alama za X kimakosa, bado kuna haja ya kuzingatia sheria na kwamba, zipo zinazoendelea kufanya kazi.

Waziri Makamba alisema serikali ya awamu ya tano imekusudia kuwatetea Watanzania wanyonge, ambao walifanyiwa makosa ya kubomolewa nyumba zao.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya wakazi wa Sharif Shamba, kutoa dukuduku lao kwa Waziri Makamba, kuhusu mradi wa ujenzi wa mfereji ulioko maeneo hayo, ambapo aliwahakikishia wananchi hao kuwa serikali imesitisha ubomoaji huo.

Mbali na hilo, Makamba alisikiliza kero za uharibifu wa mazingira unaotokana na shuguli za gereji, kando kando ya mfereji huo na kuiagiza NEMC kufika mahala hapo na kutoa maelekezo.

Aliagiza NEMC kuchukua hatua za kisheria ili kutoa maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria za uharibifu wa mazingira ili kutoa maelekezo ya kusitishwa kwa shughuli hizo.

Akitoa salamu za pongezi kwa niaba ya wakazi wa Sharif Shamba, Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonner Kalua aliishukuru serikali kwa uamuzi wa kusitisha kubomoa nyumba hizo.

Bonner alisema kitendo cha serikali kusitisha uamuzi huo ni ushujaa mkubwa wa kuwatetea Watanzania wanyonge, ambao waliwekewa kimakosa alama hizo.

Aidha, Makamba alikagua miradi ya ujenzi wa kuta kando kando ya ufukwe wa Ocean Road kwa ajili ya kudhibiti mmomonyoko wa kingo za bahari, ambapo ujenzi huo ni wa mita 828.

No comments:

Post a Comment