Monday 2 January 2017

MKURUGENZI TANESCO ATUMBULIWA, RAIS MAGUFULI ASEMA GHARAMA ZA UMEME HAZITAPANDA

RAIS Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia jana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli amemteua Dk. Tiso Mwanuka kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO na uteuzi huo unaanza mara moja.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umekuja siku chache baada ya Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), kuridhia ombi la TANESCO, kupandisha gharama za umeme nchini kwa asilimia 18.9.

Gharama hizo mpya zilipangwa kuanza jana, ambapo ilielezwa kuwa hazitawaathiri watumiaji wa nyumbani, ambao matumizi yao hayazidi uniti 75 kwa mwezi.

Mkurugenzi wa EWURA, Felix Ngamlagosi, aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa, bodi yake ilikaa na kujadili maombi yaliyoletwa na TANESCO, ambao walipendekeza umeme upande kwa asilimia 18.9

Alisema ongezeko la bei ya huduma za umeme, limetokana na kuzidi kwa gharama za uzalishaji umeme.

Hata hivyo, siku moja kabla ya gharama hizo kuanza kutumika, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliingilia kati kwa kuzuia mara moja kuanza kutumika kwake.

Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa EWURA, mwishoni mwa wiki iliyopita, Profesa Muhongo alisema amefikia uamuzi huo kutokana na mamlaka aliyonayo kisheria, hadi hapo serikali itakapopata maelezo ya kina kuhusu kupandishwa kwa gharama hizo.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Angela Sebastian ameripoti kutoka Bukoba kuwa, Rais Magufuli, amewahakikishia Watanzania kuwa licha ya EWURA kuridhia ombi la TANESCO la kupandisha bei ya umeme, kuanzia jana, bei hiyo haitapanda.

Aidha, ameupongeza uamuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kusimamisha uamuzi wa kuongeza bei ya umeme uliopitishwa na EWURA.

"Ninamshukuru sana Waziri wa Nishati na Madini kwa uamuzi wa kusitisha bei mpya. Umeme hautapanda bei, haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga viwanda, hususan katika mikakati mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka vijijini na umeme huu unaenda kwa watu masikini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake, anapandisha bei, hili haliwezekani,"alisema.

Rais Magufuli alisema amesikitishwa na uamuzi wa EWURA kutaka kupandisha kiholela bei ya umeme, bila kuzingatia hali ya uchumi kwa Watanzania huku ikishindwa pia kuwashirikisha viongozi wa juu wa serikali.

Alitoa msimamo huo jana, wakati akitoa salamu za mwaka mpya kwa niaba ya Watanzania, kwa waumini wa dinii ya kikristo katika Kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma la mjini Bukoba.

Rais Magufuli aliwaomba waumini kuwaombea laana wote wasiojali maisha ya Watanzania wanyonge na kuwanyanyasa.

Aliwaomba Watanzania kutumia sikukuu ya mwaka mpya kuliombea taifa amani kwa sababu majukumu ya kitaifa ni makubwa.

"Hata hawa waliohusika kupandisha bei ya umeme kinyemela nao ni majipu vilevile. Wamepandisha umeme, hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi. Hawakumuuliza hata waziri mwenye dhamana ya nishati. Hawakumuuliza hata makamu wa rais na waziri mkuu.

"Haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye uamuzi bila kushirikisha mamlaka nyingine. Haya Baba Askofu nayo ni majipu na mengine ni magumu kutumbuliwa, ila kwa maombi ya Watanzania tutayatumbua,"alisema.

Alisema kwa kipindi hiki ambacho taifa limejielekeza kutimiza dhamira ya kuanzisha viwanda ili kurahisisha maisha ya Watanzania wanyonge, serikali yake imejipanga kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo nchini, hivyo upandaji holela wa bei ya umeme ni kukwamisha jitihada za serikali za kufikisha nishati hiyo kwa wananchi vijijini.

Pia, aliwashauri Watanzania kumvumilia kipindi hiki, ambacho serikali imekuwa ikibana matumizi kwani kwa lengo lake ni kutaka kila mmoja apate anachostahili.

"Wanaosema serikali imeficha fedha ni waongo, fedha zilizopotea ni zile za hovyo,"alisema.

Katika mahubiri yaliyoendeshwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, alipongeza jitihada za Rais Magufuli, hususan kuhakikisha analeta usawa na uwajibikaji kwa watendaji wa serikali.

Askofu Kilaini alisema hali ya sasa kwa utendaji wa serikali imebadilika na kwamba, hivi sasa unapokwenda kwenye ofisi za umma, hakuna usumbufu wa kusubiri mtumishi wala hakuna tabia ya kuombwa kitu kidogo, kama ilivyokuwa imezoeleka kwa baadhi ya watumishi katika baadhi ya sekta.

Dk. Kilaini aliwataka Watanzania kutumia sherehe za mwaka mpya wa 2017, kujitathimini na kuondoa changamoto mbalimbali zilizojitokeza mwaka 2016, yakiwemo majanga ya tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka jana na kusababisha maafa makubwa mjini Bukoba.

“Tetemeko lililotokea Kagera sio nyundo ya kuwaumiza bali ni kengele ya kutufanya tusonge mbele, hivyo Watanzania tujielekeze kujituma kufanya kazi na asiyefanya kazi hana sababu ya kula kama yanavyosema maandiko ya kiroho”alisema.
    
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali, akiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Viwanda, Uwekezaji na Biashara, Charles Mwijage na Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama pamoja na wabunge wa majimbo ya mkoa huo.

Rais anaendelea na ziara yake ya siku mbili mkoani hapa, ambapo  leoatakagua miradi mipya inayojengwa na kuweka mawe ya msingi, ambayo ni Shule ya Sekondari ya Ihungo na Zahanati ya Kabyaile, ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi na pia atazungumza na wananchi wa Kagera.

No comments:

Post a Comment