Thursday 6 October 2016

MAHAKIMU KUPEWA MIONGOZO YA ADHABU


NA FURAHA OMARY

JAJI Mkuu, Mohammed Chande Othman, amesema mahakimu watapatiwa miongozo ya adhabu kutokana na uwepo wa utolewaji wa adhabu tofauti katika kosa moja.

Aliyasema hayo jana, Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari na Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Christopher Kourakis, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu.

Jaji Mkuu alisema wamemkaribisha  Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Kourakis ili kuzungumza na kutafuta njia za namna atakavyoshirikiana kwa ukaribu baina ya nchi hizo, kwa kuwa zote ni wanachama wa Jumuia ya Madola na zina utamaduni sawa wa kisheria.

Alisema katika mazungumzo yake na Jaji Mkuu huyo, wamekubaliana kuhusu maeneo ya ushirikiano, yakiwemo ya teknolojia za kuendesha mashauri mahakamani, mafunzo kwa majaji, wasajili na watendaji, kuanzisha kada mpya maalumu ya wapiga chapa wa mahakama na adhabu.

“Tumezungumza na kukubaliana kuhusu masuala mbalimbali, likiwemo la majaji na mahakimu wanatoa na kuangalia vipi adhabu kwa sababu, mahakama nchini tunataka kutoa miongozo ya adhabu kwa mahakimu kwani kosa hilo hilo, utakuta adhabu tofauti,”alisema.

Jaji Mkuu Chande alisema Australia Kusini ni nchi, ambayo imeendelea kiuchumi na uendeshaji wao wa mahakama umeendelea na upo wazi, hivyo Mahakama ya Tanzania inataka kujifunza kupitia kwao.

Alisema Jaji Mkuu huyo atatembelea Mahakama za Rufani, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara na atakwenda Zanzibar, ambako atakutana na Jaji Mkuu wa huko na kuzungumza naye.

Akizungumzia mambo waliyokubaliana, Jaji Mkuu Chande alisema wamekubaliana wasajili na watendaji kwenda nchini humo kujifunza namna ya kuboresha mfumo wa teknolojia kwa kuwa hapa nchini bado ni wa kutumia mikono.

“Eneo muhimu la ushirikiano ni namna ya kutumia mfumo wa teknolojia kwa kuwa mifumo yetu bado ya kutumia mikono, hivyo tunataka kuhama kwenda katika mfumo wa teknolojia,”alisema.

Jaji Mkuu Chande alisema wanataka kuanzisha kada mpya ya wapiga chapa maalumu wa mahakama, ambao watakuwa wanatumia mashine ndogo ili kuondokana na changamoto ya ucheleweshwaji wa mashauri.

Alisema nchi hiyo imeendelea kwa kuwa wapiga chapa wanapiga mwenendo wa kesi na siku hiyo hiyo unapata, jambo ambalo Tanzania hakuna, hivyo kusababisha mashauri kuchelewa.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Australia Kusini, Kourakis alimshukuru Jaji Mkuu Chande kwa mwaliko na kusema kwamba, kuna umuhimu kwa Mahakama ya Tanzania kutumia mfumo wa teknolojia kwa kuwa mashauri yanaweza kwenda haraka kwa kuwa  nyaraka zikiwemo za mwenendo wa kesi zinaweza kuchapwa na kupatikana ndani ya siku moja.

“Kupitia teknolojia, mashauri yanakwenda haraka kwa sababu jaji anapata nyaraka haraka na pia inapunguza gharama za uwepo wa mawakili,”alisema.

Jaji Mkuu Kourakis alisema kwa kutumia teknolojia nchini mwao, mashauri yanawasilishwa kwa kutumia mtandao na kuna watu wanachapa mwenendo wa kesi na kuweza kupatikana ndani ya siku moja.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, likiwemo la Australia ya Kusini walivyoweza kuondoa adhabu ya kifo, Jaji Mkuu huyo alisema adhabu hiyo ilikuwepo katika miaka ya 1970, lakini ikafutwa ambapo mtu akishitakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji, adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.

Alisema adhabu hiyo ni kifungo cha juu, ambapo cha chini ni kifungo cha miaka 20, jela bila ya kupewa Parole, lakini kuna mazingira ambayo jaji anaweza kumpunguzia adhabu mshitakiwa kama akikiri kosa.

No comments:

Post a Comment