Na waandishi wetu
MGOMBEA urais wa CCM, Dk.
John Magufuli, ameendelea kung’ara dhidi ya wagombea wa upinzani ambapo,
utafiti umeonyesha kuwa atapata ushindi
wa asilimia 66.
Huu ni utafiti wa pili
kutolewa ndani ya wiki moja, ambapo ule wa awali uliofanywa na CCM ulionyesha
Dk. Magufuli atashinda kwa asilimia 69.5 dhidi ya mgombea urais wa CHADEMA,
Edward Lowassa.
Katika utafiti huru
uliofanywa na Taasisi ya Twaweza, uliotangazwa jana mjini Dar es Salaam,
umeonyesha kuwa Dk. Magufuli bado ni kinara dhidi ya wagombea wengine.
Pia, makundi yote yakiwemo
wazee, vijana na wanawake wanamuunga mkono Dk. Magufuli kwa zaidi ya asilimia 60,
ikilinganishwa na Lowassa mwenye asilimia chini ya 28.
Pia, CCM kimeendelea kuwa
chama chenye mvuto na kilicho karibu na wananchi kwa asilimia 62, kikifuatiwa
na CHADEMA chenye asilimia 25. Vyama vingine ni na asilimia zao kwenye mabano
ni CUF (2), ACT WAZALENDO (1), NCCR-MAGEUZI (0).
Mbali na urais, pia utafiti
huo umeonyesha wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani wa CCM watapata ushindi
wa asilimia 60, wakifuatiwa na CHADEMA yenye asilimia 24.
Vyama vingine ni CUF chenye
asilimia mbili, ACT WAZALENDO na NCCR-MAGEUZI vyenye asilimia moja.
Akitangaza matokeo ya
utafiti huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TWAWEZA, Aidan Eyakuze, alisema
utafiti huo ni wa kwanza na umezingatia matakwa ya wananchi katika mikoa ya
Tanzania Bara.
Alisema utafiti huo
umefanywa kwa wananchi kupitia simu za mkononi ukiwa na uwakilishi wote wa
kitaifa.
Alisema walichukua maeneo
ya wakazi kinasibu kutoka kwenye kaya 100 ambako katika kila kaya hizo,
walimteua mtu mmoja kwa kuzingatia rika la upigaji kura.
Alisema kuwa utafiti huo
uliopewa jina la Sauti za Wananchi, ulibainisha kuwa kati ya watu watatu
waliohojiwa, wawili walisema watampigia kura Dk. Magufuli.
Hatua hiyo inatokana na
kukubalika kwa Dk. Magufuli, ambaye anaaminiwa na Watanzania wengi kutokana na
utendaji kazi wake na kutokuwa na kashfa.
Kingine ni dhamira yake
katika kupambana kulinda rasilimali za taifa na kwamba, ana uwezo wa kudhibiti
vitendo vya ufisadi ikilinganishwa na wengine.
Katika utafiti huo, pia
imebainika kuwa wananchi hawana imani na Lowassa kama ana uwezo wa kupambana na
ufisadi hivyo, hafai kuaminiwa.
Pia, utafiti huo umeonyesha
watu wote waliohojiwa wamesema Lowassa si mwaminifu hivyo, hawana imani na
hawafahamu ni kwa vipi anaweza kupambana na ufisadi.
Pia, wamesema mgombea huyo
wa CHADEMA hana tabia ya kuwajali wananchi wanyonge.
Katika kipengele hicho,
Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu kwa kashfa ya Richmond,
alipata alama sifuri.
Kwa mujibu wa Eyakuze, CCM
pia imeendelea kung’ara kwenye ngazi ya ubunge na udiwani ambapo, utafiti
umeonyesha kitapata ushindi wa asilimia 60, CHADEMA asilimia 26, CUF asilimia 3
huku ACT Wazalendo na NCCR-MAGEUZI vikishika mkia.
Pia, katika utafiti huo
asilimia mbili ya wananchi walisema bado hawajaamua watawapigia kura wagombea
wa chama gani.
Hata hivyo, utafiti huo
umeweka bayana kuwa asilimia 98 ya wananchi, wamesema wamejiandikisha kupiga
kura huku zaidi ya asilimia 99 wakionyesha dhamira ya kutumia haki yao ya kupiga kura.
Eyakuze, alibainisha kuwa
sababu za wananchi kumuunga mkono Magufuli inatokana na rekodi nzuri ya
kiutendaji, uwezo wa kutatua matatizo ya wananchi ikiwemo kupambana na ufisadi,
uaminifu pamoja na sera nzuri za chama chake.
Pia, utafiti huo
umebainisha kuwa, afya, upatikanaji wa maji, elimu na masuala ya umasikini na
uchumi, zimekuwa kero zenye kupewa kipaumbele na wananchi wakitaka zitafutiwe
ufumbuzi wa kudumu.
NAFASI YA UKAWA
Kwa mujibu wa Eyakuze,
utafiti huo umebainisha kuwa, wananchi hawaelewi nafasi ya kundi la Ukawa
kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Hali hiyo imejitokeza baada
ya asilimia 49 ya wananchi kudhani Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa
huku asilimia 57 wakitegemea kuwepo kwa jina hilo kwenye karatasi za kupigia
kura.
Hivyo kuna uwezekano wa
kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika wa maamuzi ya wapigakura kuhusiana
na kundi hilo.
Mbali na utafiti huo wa
TWAWEZA, malumbano ya ndani ya umoja huo hususan kushindwa kuzingatia
makubaliano ya mgawanyo wa mjimbo yamezua hali ya kutoaminiana.
Matokeo ya utafiti huo
yanatokana na kundi la awamu ya kwanza la wahojiwa 1,848 lililoundwa Agosti na
Septemba, mwaka huu, ambapo matokeo ya utafiti huo yanatoa picha halisi jinsi
wapiga kura wanavyowaunga mkono wagombea.
Utafiti huo haukufanyika
upande wa Zanzibar kwa sababu eneo hilo lina sheria zake zinazohusu masuala ya
utafiti hivyo, TWAWEZA haina kibali cha kuendesha tafiti kwenye visiwa hivyo.
Makamba: Utafiti haujibiwi kwa matusi
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
ya Ushindi ya CCM, January Makamba,
amewataka wote wanaobeza utafiti wa TWAWEZA kuacha kufanya hivyo kwa kuwa
utafiti wowote haujibiwi kwa matusi.
Alitoa kauli hiyo jana muda
mfupi baada ya utafiti wa TWAWEZA, ambapo alisema ni vyema wale wanaotoa
shutuma kuacha kufanya hivyo na badala yake wajikite kujibu utafiti huo kwa
utafiti mwingine na waamini CCM inapendwa mno na Watanzania.
"Tafiti yeyote
haijibiwi kwa matusi dhidi ya utafiti au mtafiti, bali jibu la tafiti ni kuja
na utafiti mbadala dhidi ya huo uliotolewa,'' alisema January.
Mbali na January, wanasiasa
wengi wameridhishwa na utafiti huo, akiwemo mgombea ubunge wa Jimbo la Nzega
Vijijini, Dk. Khamis Kigwangalla, aliyesema Watanzania wamefanya uamuzi sahihi.
Alisema utafiti wa TWAWEZA
umefanyika kwa wakati mwafaka na Watanzania, wamepata ukweli wa mambo.
Alisema utafiti huo ni
sahihi na umekuja na majawabu bora yenye mwelekeo sahihi, ambapo watanzania
wamepaza kauli zao kupitia utafiti huo, ambao ni bora.
No comments:
Post a Comment