Wednesday, 23 September 2015
MBOWE ASITAFUTE KISINGIZIO CHA KUKWEPA KUJIUZULU
NA CHARLES CHARLES
MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekituhumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kina mpango wa kung'ang'ania madarakani hata kama kitashindwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani unaofanyika baadaye mwezi ujao.
Akinukuliwa na gazeti moja litolewalo kila siku nchini, Jumapili iliyopita, Mbowe alilalamikia kauli iliyotolewa hivi karibuni na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alhaji Abdallah Bulembo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mbowe alisema kauli ya Bulembo na nyingine kadhaa, ni vitisho vinavyolenga kuvikatisha tamaa vyama vya upinzani, na pia ni kuonyesha kuwa CCM imeshapanga matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Siku chache zilizopita, Alhaji Bulembo alisema mkutanoni kuwa CCM "haiwezi kuwaachia Ikulu wapinzani", kauli ambayo kila 'mwenye kengeza la kusikia', tafsiri za hasira na jazba kama za Mbowe na viongozi wenzake wa Chadema hawawezi kuielewa kwa urahisi.
Wale ambao angalau wanaweza kuwa na uelewa kidogo bado kwa makusudi, kwa namna moja ama nyingine nao watajitahidi kwa kadri wawezavyo ili kuipotosha kwa sababu za kisiasa.
"Kama Bulembo ametoa kauli tata na viongozi hawakemei wala kuikanusha inaonyesha kuwa CCM imeshapanga matokeo, hivyo hakuna umuhimu wa kufanya uchaguzi kwa sababu uamuzi umetolewa", alisema.
Alidai pia anashangazwa na ukimya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), na kwamba vitendo hivyo vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani nchini.
"Kuliko kuingia katika uchaguzi kwa gharama za mikutano (ya kampeni) wakati wameshapanga matokeo, bora NEC itangaze kuusitisha na kumtangaza mgombea urais wa CCM kuwa mshindi", alibainisha.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa genge linaloitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema hakuna haja tena kwa vyama vya upinzani kutumia fedha (nyingi) kufanya mikutano ya kampeni nchi nzima, lakini CCM haitaki kuiachia Ikulu!
Sikuwepo jijini Dar es Salaam wakati kiongozi huyo wa Chadema alipozungumzia kauli hiyo ya Bulembo, lakini niliamini niliposoma katika gazeti hilo ambalo ni mdau mkubwa wa mgombea wa kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Chadema, Edward Lowassa.
Niliamini kwa kuzingatia ukweli kuwa gazeti hilo hivi sasa ni kama sabuni ya Lowassa, wakili wa Lowassa, mdomo wa Lowassa na dodoki la mgombea huyo wa urais aliyekimbilia Chadema ili kulazimisha kwenda Ikulu.
Sina maneno na madai hayo ya kwa sababu namjua ni bingwa wa kupotosha, mzushi na muongo aliyepo radhi na tayari hata kusema chochote, wakati wowote na mahali popote ili kukidhi matakwa yake ya kisiasa.
Sina tatizo na kauli ya Bulembo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wazazi wa CCM, hivyo namshangaa Mbowe anapokuja na madai hayo ya kitoto na kijinga kisiasa.
Nilikuwepo mkutanoni kwenye Uwanja wa Taifa wilayani Kibondo, mkoa wa Kigoma na siyo Kagera wakati Bulembo aliposema maneno hayo ya utani wa kisiasa dhidi ya Chadema, Ukawa na Lowassa kwa kuuliza maswali kadhaa likiwemo lile la kama CCM itashindwa uchaguzi huo mkuu wa rais mwezi ujao.
"Hivi ni kweli (kuwa) CCM itashindwa uchaguzi na kuiacha Ikulu kwa wapinzani?" Alihoji huku akitabasamu na kujibiwa: "Haiwezi".
Alipojibiwa swali hilo namna hiyo, Bulembo akiwa mkuu wa msafara wa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli naye aliyarudia maneno hayo kwa kusema:
"Hatuwezi tukashindwa uchaguzi na wapinzani, hatuwezi kuwaachia Ikulu kwa sababu hawawezi kutushinda maana bado ni wachanga wa kisiasa".
Hivyo ndivyo alivyosema kwa kusisitiza majibu aliyopewa na maelfu ya watu waliokuwa mkutanoni hapo.
Hivyo ndivyo alivyofanya kwa utani, lakini akasababisha Mbowe ataharuki kama mtoto wa chekeachea au kifaranga cha kuku kilichokoswakoswa na mwewe!
Nafahamu kuwa mbunge huyo wa Hai aliyemaliza muda wake anajihami. Anajua chama chake kitashindwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ifikapo mwezi ujao.
Anajua mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa hana nafasi ya kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo anachofanya ni kutafuta kisingizio chochote ambacho kitahalalisha kushindwa kwake.
Anajua mgombea urais wa chama cha Civic United Front (CUF) visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni pamoja na Chadema yenyewe, National League for Democracy (NLD) na NCCR - Mageuzi naye kamwe hatashinda.
Anajua kwamba hata yeye mwenyewe ana hali ngumu katika jimbo lake, kule ambako mwaka 2010 alishinda kwa vile CCM ilifanya kosa la kuteua mgombea ubunge, Fuya Kimbita aliyekuwa amewachosha wananchi wa Hai.
Anajua asipotafuta kisingizio chochote cha kushindwa kwa Lowassa, Maalim Seif, yeye mwenyewe, Ukawa na Chadema yake yote itakuwa 'imekula kwake' kisiasa.
Alipokuwa mkoani Lindi mwaka 2012, Mbowe aliahidi kuwa atajiuzulu shughuli zote za kisiasa na kurudi kwao endapo atashindwa kuipeleka Chadema Ikulu mwaka huu.
Nadhani ameshaona kuwa tayari utekelezaji wa ahadi yake hiyo umewadia. Badala ya miaka mitatu kama ilivyokuwa kipindi hicho sasa umebaki mwezi mmoja tu.
Nadhani anachofanya sasa ni kutafuta kisingizio chochote cha kutaka asijiuzulu.
Anataka kuipotosha kauli ya Bulembo ili awadanganye wanachama, viongozi na wafuasi wa Chadema kuwa hapaswi kujiuzulu kwa vile CCM itabaki madaraki kwa kutumia matokeo ya kupanga.
Watu wanaojua siasa na kuchanganua mambo wanaiona mbinu yake hiyo, ujanja huo na uzushi anaotaka uonekane kuwa ukweli ili asijiuzulu kwa sababu ya uchu wake wa madaraka.
Kama kauli ile ya Bulembo ina utata, vitisho na inapaswa ikemewe na kutolewa tamko na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, mbona yeye mwenyewe alikaa kimya kwa Lowassa aliposema hakuna kushindwa?
Mbona amekaa kimya kuhusu tuhuma za Chadema kupeleka zaidi ya vijana 1,500 kupata mafunzo ya 'kigaidi' huko Rwanda, wale ambao kazi yao itakuwa ni kufanya vurugu ili kuilazimisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi imtangaze Lowassa kuwa mshindi hata kama atashindwa?
Mbona amekaa kimya kwa kauli zake na viongozi wengine wa Chadema, wale wanaodai mara kwa mara kuwa mwaka huu lazima CCM ing'oke madarakani hata kama haitaki?
Kwa nini haitolei ufafanuzi kauli hiyo ili ieleweke, kwamba itatokaje madarakani kama kwa mfano itashinda?
Kwa nini hatuelezi wanaposema "hakuna kulala mpaka kieleweke" maana yake ni nini?
Nahitimisha kwa kumtaka Mbowe kuwa awe mkweli, muungwana na kuacha kutafuta visingizio vya kutaka kukwepa asijiuzulu ili kutekeleza ahadi yake ile ya mwaka 2012.
Naomba ajue kuwa kushindwa kwa Lowassa, Chadema na hata Ukawa katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani hakukwepeki iwe usiku wa manane au mchana wa jua kali.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Msaidizi, Idara ya Itikadi na Uenezi katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment