Wednesday, 23 September 2015

HAWANA UWEZO WA KUITOA CCM-SAMIA




Na Khadija Mussa, Korogwe
MGOMBEA mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema hakuna  mpinzani mwenye uwezo wa kuiondoa serikali ya CCM madarakani.
Amesema hatua hiyo inatokana na wapinzani kushindwa kuwa na wagombea wenye uwezo, hali inayosababisha kutowasilisha ilani yao kwa wananchi.
Samia amesema CCM itaendelea kubaki madarakani kutokana na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi katika sekta mbalimbali, zikiwemo za viwanda, elimu na afya.
"Mwenye nguvu ya kuishinda serikali Tanzania hii hajazaliwa, CCM tumejipanga, waje wakione," alisema alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Manundu.
Alisema duniani kote watu wanaotumia alama 'v' kama CHADEMA hawajawahi kushinda uchaguzi wowote wa kushika dola, hivyo hata UKAWA hawatashinda.
Katika hatua nyingine, Samia alisema ilani ya CCM imeweka mpango wa kuhakiki mashamba yote makubwa nchini, yakiwemo ya mkonge, ili kubaini yasiyoendelezwa na kuyarejesha kwa wananchi.
Alisema  tayari Serikali imepokea maombi kutoka maeneo mbalimbali, ikiwemo Korogwe ya kutaka kupatiwa mashamba yasiyotumika au kuendelezwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo za wananchi.
Samia alisema kufuata maombi hayo, wamepanga kuhakiki mashamba yote makubwa nchini baada ya kujiridhisha na yatakayobainika kwamba hawajaendeleza yatatolewa kwa wananchi.
Alizitaka  wilaya zote nchini, kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda kwa kuwa awamu ya tano ya uongozi wa CCM, itakuwa ni ya uchumi wa viwanda.
Alisema chama hicho kupitia ilani yake hiyo, kimeweka mikakati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, ambapo imepanga kuboresha na kuimarisha huduma muhimu kama vile maji, afya, elimu, miundombinu, ajira, viwanda, kilimo na umeme.
" Serikali pia itatenga shilingi  10 kwa ajili ya kukopesha wananchi, wakiwemo akinamama na vijana kwa ajili ya kuwawezesha, ili wajiendeleze kiuchumi," alisisitiza Samia.
Awali mgombea ubunge katika Jimbo la Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani, almaarufu  Maji Marefu, alisema jimbo lake lina tarafa nne ambazo linakabiliwa na matatizo ya ardhi, maji na kutokuwepo kwa viwanda.
"Katika tarafa ya Bungu kuna tatizo la kiwanda cha chai, pia wakulima wa chai wamepunguziwa bei ya zao hilo kutoka shilingi  276 kwa kilo hadi 176, tunaomba uingilie kati  Samia katika hili," alisisitiza.
Aidha aliomba ombi la jimbo hilo la kutaka eneo la Mombo kupandishwa hadhi na kuwa halmashauri ya mji lifanyiwe kazi pindi awamu ya tano ya Serikali ya CCM itakapoingia madarakani.
Kuhusu maslahi ya walimu, Samia alisema akiingia madarakani ataboresha maslahi ya madereva wa magari makubwa, daladala na mabasi ambao hawajapata mikataba kwa muda mrefu.
Alisema atashughulikia suala la migogoro ya  madereva ili  kumaliza mizozo ya mkataba wao wa ajira.
Samia alisema wamedhamiria kulipatia ufumbuzi suala hilo ili kuondoka migogoro ya watumishi nchini.

No comments:

Post a Comment