NA ATHNATH MKIRAMWENI
WATU wenye ulemavu wa
kusikia wamevitaka vyama vya siasa kuweka wakalimani kwenye mikutano ya hadhara,
ili kuwawezesha kufahamu sera na ahadi zinazozungumziwa na wagombea.
Wamesema mikutano mingi ya
kampeni ya vyama vya siasa haina wakalimani, hali inayowafanya washindwe
kushiriki kikamilifu na badala yake kuwa wasindikizaji, licha ya kwamba
wanapiga kura kuchagua viongozi.
Kauli hiyo imetajwa kuwa ni
changamoto kubwa kwa jamii hiyo, kwanihawatambui kinachosemwa na wagombea
kuanzia urais, ubunge na udiwani.
Ofisa Jinsia na Maendeleo
wa Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Lupi Maswanya, alisema ili washiriki
ipasavyo mikutano ya kampeni, suala la vyama kuweka wakalimani ni la
msingi.
Alisema kutokana na
changamoto hiyo, wameandaa Maadhimisho ya Siku ya Walemavu yaliayoanza jana na
kilele chake kitakuwa Septemba 27, mwaka huu.
Alisema lengo la
maadhimisho hayo ni kusisitiza
ujumuishaji wa haki za matumizi lugha ya alama nchini kwa watoto viziwi, ili wanufaike na
elimu na fursa nyingine za kijamii.
Lupi alisema maadhimisho
hayo yamebebwa na kauli mbiu isemayo ‘Kwa haki za lugha ya alama ya Tanzania
watoto wetu wanaweza kuihamasisha jamii
kutambua mchango wa viziwi, haki za binadamu na maandalizi ya viziwi katika
kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha’.
“Kwa haki ya lugha ya alama
watoto wetu wanaweza kutambua lugha za
alama kwa njia halali ya kiisimu ya kuwasilisha mawazo, fikra na hisia za
kujadili mijadala mbalimbali,’’ alisema.
Naye Ofisa Uhusiano Umoja
wa Miradi kwa Viziwi (UMITA), Tungi Mwanjala, aliiomba serikali kuwatengenezea
walemavu vitambulisho maalum vitakavyowatambulisha siku ya kupiga kura ili nao
kushiriki ipasavyo kuchagua kiongozi makini.
‘’Watu wasioona
wametengenezewa utaratiu wa kusoma kwa kutumia nukta nundu, lakini sisi tusiosikia hatujatengenezewa mazingira rafiki
kutuwezesha kushiriki kupiga kura, basi
tutengenezewe vitambulisho maalumu vya kututambulisha,’’ alisema.
Maadhimisho hayo
yanafanyika mkoani Pwani, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid.
No comments:
Post a Comment