NA
PETER KATULANDA, KALIUA
WATANZANIA
waliopata urai mpya wilayani hapa, baada ya kuhamia kutoka Burundi, wameahidi kuipigia kura za kishindo
CCM, akiwemo mgombea wake wa urais, Dk. John Magufuli.
Wamesema
licha ya kushawishiwa na wagombea wa vyama vingine, akiwemo Mwenyekiti wa chama
cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, wasiipigie kura CCM, wataipigia kura zao zote
na hakuna mwingine wanayetamani awe rais wa Tanazania zaidi ya Dk. Magufuli.
Ahadi
hiyo waliitoa juzi kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni za mgombea
ubunge wa CCM katika Jimbo la Ulyankulu, John Kadutu, iliyofanyika katika
vijiji vya Mtakuja, Keza, Imara na Taba Kata ya Igombemkuru, wilayani Kaliua,
mkoani Tabora.
“Toka
mwaka 1972 wazazi wetu walipokimbia Burundi na kupewa makazi hapa Keza,
kulikuwa na chama kimoja tu cha CCM, wamezeekea hapa, wengine wamefia hapa na
sisi wengine tumezaliwa hapa, hata uraia tumepewa na serika ya CCM.
Tunamshukuru Rais Jakaya Kikwete,” alisema Midiam Tito.
Tito,
mkazi wa Keza na Katibu wa CCM wa Kata hiyo, alisema yeye na raia wenzake
wapya, wote watakipigia kura Chama Cha Mapinduzi ambacho kimekuwa na uongozi bora
na kimetunza amani ya Tanzania.
“Kwani
Rais Kikwete angekataa tusipewe uraia nani angemlazimisha,” alihoji Adoneth Dotto.
Adoneth
alisema wana matumaini na mapenzi makubwa kwa CCM na kwamba tangu akiwa mdogo, wazazi wake walimwambia CCM
wasingelinda amani na kusaidia nchi nyingine, wasingekuwa hai na asingezaliwa.
Wakimkaribisha
Kadutu kwa shangwe, vifijo, vigelegele na nyimbo za kumpongeza Dk. Magufuli
katika vijiji vya Imara na Taba, raia hao walisema wiki iliyopita, Zitto aliondoka kwa aibu baada ya kukosa watu wa
kumsikiliza kabla ya kwenda kuhutubia Ulyankulu, ambapo pia alipata watu wachache.
Walisema
wanatamani Dk. Magufuli awatembelee na kuona makazi yao ambayo kutokana na
kutokuwa na uhakika wa kuishi (kabla ya kupewa uraia) kwa miaka 10, walishindwa
kuyaendeleza, lakini sasa kwa kuwa wamekuwa Watanzania halali, watachapa kazi
wapate maendeleo.
Watanzania
hao ambao kutokana na kutosajiliwa mapema kwa Kata yao, hawataweza kupiga kura
za madiwani, waliahidi kumpa kura nyingi Kadutu na kudai kuwa wagombea wa UKAWA,
akiwemo Edward Lowassa, wasipoteze muda wao kwenda kuwaomba kura, kwani watamtazama kama walivyomfanyia Zitto.
Akizungumza
na wananchi hao, Kadutu alisema Rais Kikwete kama alivyokuwa Hayati Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, anapenda watu, atakumbukwa kwa mengi, likiwemo la wao
kupewa uraia.
Aliwaomba
wananchi hao kuichagua CCM ili washirikiane kujenga nchi na kuwaletea maendeleo,
ambapo aliahidi kufufua na kuboresha barabara za awali wakati wa makazi ya raia
hao walipokuwa wakimbizi.
Aidha,
atashirikiana na wananchi hao kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu,
zahanati na kwa kuanzia ,atatoa mifuko 300 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa
shule ya Msingi Mwankuba na kujenga nyumba moja ya walimu katika Kijiji cha
Taba.
Kadutu
alisema ubora wa Dk. Magufuli hauwezi kulinganishwa na wa wagombea wengine
wanaosaka urais.
Watanzaia
hao wapya walipewa uraia Aprili, 2014, baada ya kuishi nchini kwa zaidi ya
miaka 40 tangu mwaka 1972 walipokimbia machafuko ya mapigano ya wenyewe kwa
wenyewe nchini Burundi na wengine kuzaliwa nchi hapa baada ya wazazi kukimbia.
No comments:
Post a Comment