Wednesday, 23 September 2015
MCHAGUENI DK. MAGUFULI- MAKAMBA
NA KHADIJA MUSSA, TANGA
WATANZANIA wametakiwa kumchagua mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ili taifa liendelee kuwa katika mikono salama.
Pia wametakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kutoogopa vitisho vinavyotolewa kwa kuwa vyombo vya dola vimejipanga kisawa sawa katika kuimarisha ulinzi.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika katika viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
January alisema ni lazima watu waangalie ni mtu wa aina gani anayefaa kupewa nafasi ya kuongoza nchi kwa sababu wengine hawana uwezo na wanaweza kulipeleka taifa pabaya, hivyo Oktoba 25, mwaka huu, wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuichagua CCM.
"Nchi itakuwa salama katika mikono ya Dk. Magufuli na mama Samia. Mkiwapa watu wengine nchi itaingia shakani, chagueni CCM kwa kuwa ndicho chama pekee chenye lengo la kuwaletea maendeleo," alisema.
Katika hatua nyingine, January aliwaomba wanawake kutumia fursa waliyopewa kwa kuonyesha kuwa wanaweza kwa kumchagua Dk. Magufuli kuwa rais na kumwezesha Samia kuwa Makamu wa kwanza wa Rais mwanamke.
Alisema itakuwa ni bahati kwa nchi kuwa na makamu wa rais mwanamke, ambaye ni mweledi na ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi.
Kwa upande wake, Samia alisema atahakikisha tatizo la maji linamalizika nchini ili kuwaondolea kinamama adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
"Mimi ni mama, najua shida mnayopata wakina mama ya kwenda umbali mrefu kutafuta maji. Nitasimamia kwa uwezo wangu wote kuhakikisha kila eneo linapata maji," alisema.
Alisema tatizo la maji litakuwa kipaumbele chake cha kwanza kufanyia kazi atakapoingia madarakani.
Samia aliwaomba wananchi kumpigia kura Dk. Magufuli, ili yeye awe makamu wa rais na kusema kwamba CCM imejipanga kutatua matatizo ya wananchi.
Aliwahakikishia wananchi hao kwamba CCM ipo tayari kutatua matatizo ya ardhi katika mkoa huo na kurudisha mashamba yasiyoendelezwa kwao.
"Tunajua kuna mashamba ambayo wamepewa wawekezaji, lakini hawajaendeleza, tutayarudisha kwa wananchi ili wayatumie kwa kilimo," alisema.
Samia alisema kurudishwa mashamba hayo kutasaidia kuinua wananchi kiuchumi kupitia kilimo, ambapo pia aliwaomba wajitume na kufanya kazi ili kuongeza kipato.
Akizungumzia suala la masoko, Samia alisema watajenga masoko mapya na vituo vipya vya mabasi ambayo vitakuwa na maengesho ya pikipiki na bajaji katika kuendelea kuinua mwananchi kiuchumi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment