Wednesday, 23 September 2015

SAMIA AVUNA WANACHAMA 600 WA UPINZANI


Na Khadija Mussa, Tanga
MGOMBEA Mwenza wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ameusambaratisha upinzani mkoani hapa, baada ya kuzoa wanachama zaidi ya 600 kutoka vyama vya CUF, CHADEMA na ACT-WAZALENDO.
Wanachama hao waliamua kujiunga na CCM wakati wa mikutano ya kampeni ya Samia, iliyofanyika katika maeneo ya Usagara, jijini Tanga, Muheza, Korogwe mjini na Pongwe.
Katika mkutano wa Korogwe Mjini, Mwenyekiti wa Kata Mswaha kutoka CUF pamoja na wanachama wenzake 280 kutoka chama hicho na Mwenyekiti wa CHADEMA kutoka Kata ya Chagunda, walijiunga na CCM.
Akizungumza  baada ya kupokea wanachama hao, Samia alisema wanachama hao wameshituka baada ya kubaini walikuwa wamepotea kwa kwenda upinzani na kuamua kujiunga na CCM.
"Msiwaite wapinzani tena kwa sababu hawa si wapinzani, wameshituka na kuamua kurudi nyumbani katika chama kinachoeleweka, hivyo naomba tuwape ushirikiano ili kwa pamoja tupate ushindi wa kishindo," alisema.
Katika hatua nyingine, Samia alisema serikali ya awamu ya tano itaboresha maslahi ya watumishi wa umma kwa kufanya mapitio ya mishahara, ili ilingane na gharama za maisha.
Kuhusu suala la wananchi wa Wilaya ya Korogwe kukabiliwa na changamoto ya maeneo ya makazi na kilimo, alisema atawasiliana na uongozi wa halmashauri kuangalia namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Awali, mgombea ubunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, Mary Chatanda, alimwahidi Samia ushindi wa kishindo kwa nafasi zote, ambapo alimwomba akiingia madarakani awasaidie katika kutatua kero zinazowakabili, zikiwemo za miundombinu, maji safi na salama pamoja na ujenzi wa hospitali.

No comments:

Post a Comment